NCHI ZA AFRIKA ZIMEKUBALIANA KUWEKA KIPAUMBELE KATIKA UFADHILI WA VIWANDA VINAVYOTEGEMEA RASILIMALI ZA NDANI



Nchi za Afrika zimekubaliana kuweka kipaumbele katika ufadhili wa viwanda vinavyotegemea rasilimali za ndani ikiwemo madini na kuhakikisha kuwa zinaongeza thamani ya bidhaa na kuimarisha biashara ya ndani ya bara ili kujenga maendeleo jumuishi, endelevu na yenye tija.

Naibu Waziri wa Fedha Mhandisi Mshamu Ali Munde amesema hayo baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Pamoja wa 9 wa Kamati Maalum ya Mawaziri ya Umoja wa Afrika inayosimamia masuala ya Fedha, Uchumi, Mipango na Mtangamano pamoja na Mkutano wa 5 wa Kamati Maalum ya Mawaziri inayosimamia masuala ya Biashara, Utalii, Viwanda na Madini, uliofanyika jijini Abidjan, nchini Ivory Coast.

Mhandisi Munde amesema hatua hiyo inalenga kuharakisha mageuzi ya uchumi kwa kuongeza thamani ya rasilimali zilizopo, kuimarisha ushirikiano wa kikanda ili kupunguza utegemezi kutoka kwa wafadhili.

Awali akizungumza wakati akichangia mada, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo amesema ili kuharakisha mageuzi ya kiuchumi Afrika ni muhimu kuimarisha ujumuishaji wa kifedha, kuendeleza shoroba za kiuchumi, pamoja na kuweka mifumo bora ya usafirishaji na ugavi ili kuongeza ushindani katika masoko ya kikanda na ya kimataifa.






No comments