SERIKALI ZOTE MBILI ZA TANZANIA, ZINAENDELEA KUTHAMINI NA KUWEKEZA KATIKA LUGHA YA KISWAHILI



Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dokta Riziki Pembe Juma amesema Serikali zote mbili za Tanzania, zinaendelea kuthamini na kuwekeza katika lugha ya Kiswahili.

Amesema lugha hiyo imekuwa rasmi na inatumika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC na Umoja wa Afrika ambapo inazidi kupata nafasi katika Taasisi mbalimbali za Kimataifa ikiwemo, UNESCO.

Dokta Riziki amesema hayo wakati wa Maadhimisho ya miaka 10 ya Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Kiswahili ya Fasihi ya Afrika iliyofanyika Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

Amesema mafanikio hayo, yanahitaji kuendelezwa kwa kuzalisha kazi bora za fasihi ili kiswahili kiendelee kuwa lugha ya Elimu, Tafiti, Ubunifu na Diplomasia kama walivyosema wahenga Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Habari Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar Matar Zahor Masoud amesema lugha ya kiswahili ni Tunu ya Taifa na adhimu, hivyo Viongozi na Wananchi wanapaswa kuitunza na kuiendeleza ili isaidie katika kunyanyua Uchumi wa Nchi na Bara la Afrika kwa Ujumla.

Tuzo hizo kwa mwaka 2026, zimeshirikisha mashindano ya Hadithi fupi fupi, Riwaya na Ushairi ambapo washindi wa  kwanza kwa kila tunzo wamezawadiwa Dola 5,000.







No comments