DKT GRACE MAGEMBE AONGOZA KIKAO CHA MENEJIMENTI YA WIZARA YA AFYA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe, leo Agosti 13, 2026 ameongoza kikao cha Menejimenti ya Wizara ya Afya, kilicholenga kupitia ajenda zilizojadiliwa katika kikao kilichopita pamoja na kujadili ajenda mpya zinazolenga kuimarisha utendaji na ufanisi wa Wizara pamoja na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.
Miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa ni pamoja na uwasilishaji wa Taarifa ya Tathmini ya Utendaji wa Idara, Vitengo, Mabaraza na Programu, pamoja na Taarifa ya Utekelezaji wa Kampeni ya Chanjo ya Polio nchini.
Aidha, kikao hicho pia kimejadili Mwongozo wa Kitaifa wa Uanzishaji, Uendeshaji na Usimamizi wa Klabu za Afya na Lishe katika Shule za Msingi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha afya na lishe kwa watoto shuleni.
Vilevile, Menejimenti imejadili masuala muhimu yanayohusiana na utekelezaji wa ajenda za kisekta, ikiwemo Sheria ya Afya, Sera ya Afya na Bima ya Afya kwa Wote, kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wake unakwenda sambamba na mipango na vipaumbele vya Serikali katika kuboresha huduma za afya nchini.








Post a Comment