JAJI MSHIBE ASISITIZA MAANDALIZI YA KISEKTA KUKABILIANA NA ATHARI ZA EL NIÑO
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Jaji Mshibe Ali Bakari, amezitaka sekta zote kutumia ipasavyo taarifa za hali ya hewa katika kufanya maandalizi ya kisekta ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na uwepo wa El Niño.
Jaji Mshibe, amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa 25 wa kujadili Utabiri wa Msimu wa Mvua za Vuli, Oktoba hadi Disemba 2026, uliofanyika jijini Dodoma.
Tanzania, kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani, inaendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa yanayodhihirishwa kupitia ongezeko la joto, ukame, upepo mkali, vimbunga na vipindi vya mvua kubwa vinavyoweza kusababisha mafuriko, hivyo wadau wametakiwa wasiishie katika kupokea taarifa za utabiri wa hali ya hewa, bali wazitumie katika kufanya maamuzi yanayozingatia mazingira ya sekta na maeneo yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a, alisema TMA imeendelea kuboresha utoaji wa taarifa za hali ya hewa, ikiwemo kuandaa utabiri mahususi kwa maeneo madogo kwa wilaya 86 zilizopo katika mikoa inayopata mvua za Vuli, hatua inayolenga kuhakikisha kila wilaya na sekta husika zinaweza kutumia taarifa za hali ya hewa katika kufanya maamuzi na kupanga shughuli zao.
Naye, mwakilishi wa wadau mbalimbali kutoka Zanzibar, Makame K. Makame, Mkurugenzi wa kamisheni ya kukabiliana na maafa Zanzibar, alisema "Utabiri wa hali ya hewa ni jambo moja muhimu mno hasa katika kipindi cha El -Nino ambapo jamii na sekta zote muhimu zinahitaji kujikinga, kujiandaa, kukabiliana na majanga au maafa yanayoweza kutokea sambamba na kurejesha hali baada ya maafa".
TMA inatarajia kutoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Vuli 2026 tarehe 18 Agosti 2026.

Post a Comment