KAMATI YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII YARIDHISHWA NA UTENDAJI WA TFS PAMOJA NA USIMAMIZI MZURI WA WIZARA



Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeeleza kuridhishwa na utendaji wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na kuwataka kufanya maboresho katika matumizi ya mifumo ya ukusanyaji wa mapato ili kuzuia mianya ya upotevu wa mapato.


Akizungumza mara baada ya Kamati hiyo kupokea na kujadili taarifa ya utendaji kazi  wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa mwaka wa fedha 2025/2026 na mafanikio yake katika kikao kilichofanyika Agosti 19, 2026 Jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Timotheo Mnzava (Mb), ameupongeza uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuzismamia vyema taasisi zake.


Mhe. Mzava ameitaka TFS kuendelea kusimamia sheria na taratibu ili kulinda na kuendeleza misitu sambamba na kuboresha mahusiano na jamii inayozunguka misitu hiyo sambamba na kuishirikisha katika uhifadhi, ulinzi na uendelezaji wa pamoja kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.


Pia ameitaka TFS kuboresha na kuendeleza uwekezaji katika vivutio vya utalii vinavyosimamiwa na mamlaka hiyo sambamba na kuboresha miundombinu katika maeneo ya utalii ili kuvifanya vivutio hivyo kufikika kwa urahisi na kuwavutia watalii wengi zaidi jambo litakaloongeza mapato ya serikali.


Awali akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya kamati hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), amesema Wizara itaendelea kushirikiana na kamati hiyo katika kufikia malengo ya Serikali huku ikitambua jukumu la uhifadhi wa rasilimali na kuongeza thamani katika mazao yatokanayo na Misitu iliyopo hapa nchini kwa ajili ya urithi wa kizazi cha sasa na kijacho. 


Dkt. Kijaji ameyataja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika Wizara kupitia TFS kuwa ni kuimarika kwa uhifadhi Misitu na Ufugaji Nyuki, kuongezeka kwa  idadi ya watalii na Utalii wa Misitu ya asili hali iliyosababisha ongezeko la  ukusanyaji wa mapato na maduhuli pamoja na kutoa hati miliki za Kimila kwa jamii ya wakazi ya Mkoa Tabora katika Halmashauri ya Wilaya ya Urambo na Sikonge.


Kikao hicho kimehuduriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), Naibu Katibu Mkuu Bw. Nkoba Mabula, Menejimenti ya Wizara na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).















No comments