SERA NA SHERIA ZA AFYA KUIMARISHA MFUMO WA KUSIMAMIA UBORA WA HUDUMA



Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanya mapitio ya Sera ya Afya ya Mwaka 2007 ili kuhakikisha sera hiyo inaendana na mabadiliko yaliyopo katika sekta ya afya pamoja na mahitaji ya wananchi kwa sasa na miaka ijayo.


Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Florence Samizi, amesema hayo leo Agosti 14, 2026 akimwakilisha Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, wakati akiwasilisha taarifa kuhusu Sera ya Afya ya Mwaka 2007 na Sheria ya Usimamizi wa Huduma za Afya mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, katika Kumbi za Bunge, Dodoma.


“Utekelezaji wa Sera ya Afya ya Mwaka 2007 umewezesha kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, ambapo takribani asilimia 80 ya Watanzania wanaweza kupata huduma za afya ndani ya umbali wa kilomita tano, pamoja na kuchangia kupungua kwa vifo vya uzazi na watoto chini ya miaka mitano,” amesema Dkt. Samizi.


Aidha, Dkt. Samizi amesema Serikali inalenga kuweka mfumo utakaosimamia ubora wa huduma za afya, kulinda haki za wagonjwa na kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma kwa usawa bila kujali hali yake, huku changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utoaji wa huduma zikishughulikiwa ipasavyo.


Amesema Serikali pia, itaendelea kuimarisha usimamizi wa taaluma na uwajibikaji wa wataalamu wa afya ili kuhakikisha makosa ya kitaaluma yanashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu na sheria, bila kuathiri haki za wagonjwa.


Akifafanua kuhusu taarifa hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, amesema moja ya maeneo muhimu yaliyoboreshwa ni ugharamiaji wa huduma za afya kupitia utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, huku Serikali ikiweka utaratibu wa kuwagharamia wananchi wasio na uwezo.


Dkt. Magembe amesema Wizara pia imeanza mchakato wa kuweka mfumo madhubuti wa kisheria wa kusimamia utoaji wa huduma za afya nchini, ikiwemo kutambua mamlaka ya Ofisi ya Mganga Mkuu wa Serikali na kuanzisha chombo cha kusimamia ubora na ithibati ya huduma za afya.


Mwisho, Dkt. Magembe amesema wamepokea maoni, ushauri na michango ya Wabunge kuhusu Sera ya Afya na Sheria ya Usimamizi wa Huduma za Afya ambayo itayazingatia katika kuhakikisha mifumo hiyo inaendana na mahitaji ya wananchi na mabadiliko yanayotokea katika sekta ya afya.


















No comments