TANZANIA YAONGOZA AFRIKA MASHARIKI KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA WATOTO
Tanzania imeeleza hatua kubwa iliyopiga katika kupunguza vifo vya akina mama, watoto wachanga na watoto chini ya miaka mitano, huku ikisisitiza kuwa uwekezaji endelevu katika huduma za afya ya msingi ni hatua muhimu ya kuhakikisha kila mama anajifungua salama na kila mtoto anapata fursa ya kuishi na kukua.
Akizungumza Agosti 18, 2026 katika Mkutano wa Nne wa Kamati ya Uongozi ya Mawaziri wa Afya wa Kanda ya Afrika Mashariki (ReSCO), uliofanyika Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa (Mb.), ambaye alikuwa Mwenyekiti wa mkutano huo, amesema kati ya asilimia 80 hadi 85 ya Watanzania sasa wanaweza kupata huduma za afya, ikiwemo afya ya mama na mtoto, ndani ya kilomita tano kutoka wanapoishi.
Amesema upanuzi wa huduma za Afya umeenda sambamba na ongezeko la vituo vya huduma za watoto wachanga kutoka 14 mwaka 2018 hadi 438 mwaka 2025, huku kiwango cha vifo vya uzazi vikishuka kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 kati ya mwaka 2015 na 2022. Katika kipindi hicho, vifo vya watoto chini ya miaka mitano vilipungua kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000.
Mhe. Mchengerwa amesema mafanikio hayo yamechangiwa na kuimarishwa kwa huduma za afya ya msingi, huduma za kujifungua katika vituo vya afya, mifumo ya rufaa za dharura kupitia m-mama, kuongezeka kwa watoa huduma wenye ujuzi pamoja na matumizi ya teknolojia kupitia teleconsultation na mifumo ya kidijitali ya kufuatilia vifo vya mama na watoto.
Aidha, amesema Tanzania imeendelea kuwalinda watoto dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa kudumisha kiwango cha chanjo cha zaidi ya asilimia 95, sambamba na hatua za kudhibiti malaria na kuendelea kupiga hatua katika mapambano dhidi ya VVU. Ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa mstari wa mbele katika ajenda hiyo kupitia kampeni ya "Jiongeze Tuwavushe Salama".
Amesema mafanikio hayo yanaonesha kuwa uwekezaji wa muda mrefu katika huduma za afya ya msingi, miundombinu, wataalamu na bidhaa muhimu za afya unaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vinavyoweza kuzuilika, akisisitiza kuwa hakuna mwanamke anayepaswa kufariki wakati wa kujifungua na kila mtoto anapaswa si tu kuishi, bali astawi.
Kwa upande wa Afrika, Mhe. Mchengerwa amezitaka nchi za Afrika Mashariki kuongeza uwekezaji unaotabirika na wa kibunifu katika afya ya mama, mtoto na huduma za afya ya msingi, akieleza kuwa afya ya mama na mtoto ni kipimo cha uimara wa mifumo ya afya na maendeleo ya taifa. Mkutano huo umejadili namna ya kuimarisha usalama wa afya na kujitegemea katika afya kupitia uwekezaji katika maeneo hayo.
.jpeg)



.jpeg)
Post a Comment