JESHI LA MAGEREZA KUTUMA WAWAKILISHI MKUTANO WA KIMATAIFA WA ASKARI WANAWAKE NCHINI INDONESIA
Jeshi la Magereza limekabidhi Bendera ya Taifa kwa maafisa wawili Wanawake wanaotarajiwa kuliwakilisha Jeshi la Magereza katika Mkutano wa Kimataifa wa Polisi Wanawake Duniani (IAWP), utakaofanyika jijini Bali, Indonesia.
Hafla hiyo ya kukabidhi bendera imefanyika Septemba 11, 2026, ambapo Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano ya Kimataifa wa Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) Themistocles Timothy Ifunya, amewaaga rasmi maafisa hao kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Yoram Katungu.
Wajumbe walioteuliwa kuipeperusha Bendera ya Tanzania katika jukwaa hilo la kimataifa ni Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Edith Mbogo pamoja na Sajini (SGT) Elizabeth Haule.
Mkutano huo mkubwa unaoleta pamoja wanawake walio katika vyombo vya ulinzi na usalama kutoka mataifa mbalimbali duniani, unatarajiwa kuanza rasmi Septemba 20, 2026.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, SACP Ifunya amewataka maafisa hao kuwa mabalozi wazuri, kushiriki kikamilifu katika majadiliano, na kuhakikisha wanatumia fursa hiyo kujenga na kuimarisha diplomasia pamoja na mahusiano ya kimataifa ya kiusalama kwa maslahi ya Jeshi la Magereza.
Mkutano wa IAWP hufanyika kila mwaka kwa lengo la kubadilishana uzoefu, mbinu za kisasa za kupambana na uhalifu, na kukuza nafasi ya uongozi kwa wanawake ndani ya vyombo vya dola ulimwenguni.

Post a Comment