JESHI LA MAGEREZA TANZANIA KUANDAA MPANGO WA UWEKEZAJI NA SEKTA BINAFSI

Jeshi la Magereza limeanza mikakati ya kufungua milango ya uwekezaji kwa kushirikiana na sekta binafsi, katika hatua inayolenga kuongeza tija na kuboresha utendaji wa Jeshi kupitia Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).


Mkuu wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Katungu, Septemba 11, 2026, amefanya mazungumzo rasmi na Kaimu Kamishna wa PPP kutoka Wizara ya Fedha, Ndg. Bashiru Hussein Taratibu, Makao Makuu ya Jeshi la Magereza yaliyopo Msalato, jijini Dodoma.


Mazungumzo hayo yamelenga kuainisha na kujadili namna bora ya utekelezaji wa miradi ya uwekezaji itakayo shirikisha taasisi binafsi, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuimarisha uchumi kupitia mifumo ya PPP.


Katika ziara hiyo ya kikazi, Kaimu Kamishna Taratibu ameambatana na wataalamu wa uchumi kutoka Wizara ya Fedha , akiwemo Mchumi Mkuu wa PPP, Ndg. Lafred Misana, pamoja na Mchumi, Bi. Anastazia Amandi, ili kutoa miongozo ya kitaalamu na kisheria namna ya kuendesha uwekezaji huo kwa ufanisi.


Jeshi la Magereza nchini limekuwa likijihusisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji, ikiwemo kilimo, ufugaji, na viwanda vidogo vidogo. Ushirikiano huu mpya unatajwa kuwa fursa muhimu itakayoruhusu mitaji na teknolojia kutoka sekta binafsi kuongeza nguvu katika maeneo hayo ya kimkakati.

No comments