MASHILI AKABIDHI MSAADA WA KICHOMEA TAKA NA JENERETA CHUO CHA UUGUZI NZEGA



Mkurugenzi Mtendaji wa Mashili Company Limited Peter Mashili, ametekeleza ahadi aliyoitoa Agosti 7, 2026 wakati alipokuwa mgeni rasmi katika Mahafali ya Nne ya Chuo cha Uuguzi na Ukunga Nzega, kwa kukabidhi kichomea taka alichokijenga kwa gharama ya shilingi Milioni 6.9 pamoja na jenereta ambalo amelinunua shilingi milioni 4.2.


Akikabidhi mchango huo leo kwa Mkuu wa Chuo cha Uuguzi na Ukunga Nzega, Josephat Kaja, Mashili amesema utekelezaji wa ahadi hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha elimu na mafunzo ya wataalamu wa afya, sambamba na kuboresha mazingira ya wanafunzi na wakufunzi.


Mashili amesema vifaa hivyo vyote vilivyogharimu shilingi milioni 11.186 ili ni maalumu kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za umeme na kuboresha mazingira ya chuo.


Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Nzega, Zalna Dickolagwa, amemshukuru Mashili kupitia kampuni yake inayojihusisha na uchimbaji wa madini kwa kuendelea kufanya shughuli za uwekezaji huku akitambua umuhimu wa kurudisha sehemu ya mafanikio kwa jamii kupitia Uwajibikaji kwa Jamii (CSR). 


Mchango huo unakuja ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali za kuongeza idadi ya wataalamu wa afya nchini kupitia vyuo vya mafunzo, wakati Chuo cha Uuguzi na Ukunga Nzega kikiwa na wanafunzi 143, wakiwemo wasichana 93 na wavulana 50.







No comments