RUWASA YATAKIWA KUHARAKISHA HUDUMA YA MAJI VIJIJI 1,575.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji,Rose Ambrose ameutaka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA),kuharakisha utekelezaji wa mpango wa kufikisha huduma ya maji katika vijiji 1,575 ambavyo bado havina huduma hiyo.
Amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa changamoto ya ukosefu wa maji katika vijiji hivyo inaathiri zaidi akina mama na watoto wanaolazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji, hali inayowafanya kushindwa kufanya shughuli za kuendeleza kaya zao na watoto kushindwa kuhudhuria masomo ipasavyo.
Akizungumza katika Kikao Kazi cha Bodi ya Wakurugenzi na Watendaji wa RUWASA kinachofanyika Septemba 9 hadi 11, 2026 katika Ukumbi wa Jenerali Mabeho jijini Dodoma, amesema Wizara ya Maji inaitazama RUWASA kama chombo muhimu katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma bora na endelevu ya maji safi na salama.
Kwa mujibu wa hotuba hiyo, RUWASA tayari imefanikiwa kutekeleza miradi ya maji na kufikisha huduma kwa zaidi ya asilimia 85 ya wananchi wanaoishi vijijini, huku ikielekezwa kuanza utekelezaji wa mpango wa kufikisha huduma katika vijiji 1,575 visivyokuwa na huduma hiyo.
Ametaka watendaji wa RUWASA kutokuwa sehemu ya malalamiko na visingizio, bali kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto zinazowakabili, huku wakishirikiana na Wizara ya Maji, Sekretarieti za Mikoa, Halmashauri za Wilaya, Vyombo vya Utoaji Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs) pamoja na wadau wengine katika mnyororo wa huduma ya maji.
Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Wolta Kirita amesema, wakala huo ulioanza miaka saba iliyopita umepata mafanikio mengi yakiwemo ya kusambaza maji vijijini na vimebaki vijiji 1,575 tu na ili kuhakikisha vijiji hivyo vinapata huduma ya maji zinahitajika Sh trilioni 5.1.
Post a Comment