WANAFUNZI SHULE ZA MSINGI DARASA LA SABA KUFANYA MITIHANI YA TAIFA KESHO NA KESHOKUTWA
Watahiniwa 1,168,649 kutoka shule 20,019 nchini wanatarajiwa kuanza kufanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) kesho Septemba 9 na 10, 2026.
Kati ya watahiniwa hao, wavulana ni 531,467 sawa na asilimia 45.48, huku wasichana wakiwa 637,182 sawa na asilimia 54.52. Aidha, watahiniwa 4,867 wenye mahitaji maalum wamesajiliwa kufanya mtihani huo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 8, 2026, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Profesa Said Ally Mohamed, amesema maandalizi ya mtihani huo yamekamilika na karatasi pamoja na nyaraka muhimu za mitihani zimesambazwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Amesema watahiniwa 1,081,204 sawa na asilimia 92.52 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili, wakati 87,445 sawa na asilimia 7.48 watafanya kwa lugha ya Kiingereza.
Profesa Mohamed amewataka watahiniwa kuzingatia kanuni za mitihani na kujiepusha na vitendo vya udanganyifu, akisisitiza kuwa matokeo ya mtahiniwa atakayebainika kufanya udanganyifu yatafutwa.
Aidha, amezitaka Kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri kuhakikisha usalama wa vituo unaimarishwa, huku jamii ikihimizwa kutoa taarifa kuhusu vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha uendeshaji wa mtihani huo.

Post a Comment