Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Kituo cha Afrika cha Mageuzi ya Kiuchumi



Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Kituo cha Afrika cha Mageuzi ya Kiuchumi (African Centre for Economic Transformation – ACET), ukiongozwa na Rais wa Kituo hicho, Bi. Mavis Owusu Gyamfi, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (World Bank Group), inayofanyika jijini Bangkok, nchini Thailand.


Katika mazungumzo hayo, walijadili  kuanzisha ushirikiano katika masuala ya mageuzi ya kiuchumi, ikiwemo kufanya uchambuzi wa hali ya uchumi na vipaumbele vya maendeleo ya Tanzania, kutafuta rasilimali za kusaidia utekelezaji wa mapendekezo yatakayotolewa, pamoja na kuweka mifumo ya kufuatilia maendeleo na kupima matokeo ya utekelezaji.


Ushirikiano huo unalenga kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuharakisha mageuzi ya kiuchumi na kukuza maendeleo endelevu, kwa kushirikiana na taasisi za ndani ya nchi na wadau wa maendeleo kupitia uongozi wa Serikali ili kuhakikisha umiliki na uendelevu.



Mkutano huo ulilenga kuoanisha mfumo wa ACET wa Growth with Depth na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 pamoja na lengo lake kabambe la kuwa uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.


ACET, ni Taasisi huru ya utafiti wa sera iliyo na makao yake makuu mjini Accra, Ghana, ambayo katika mkutano huo ilipendekeza utekelezaji wa Country Economic Transformation Outlook (CETO) unaohusisha uchambuzi wa kina wa data za uchumi wa nchi ili kubaini fursa na hatari mahususi ambapo ilisistiza kwamba mbinu yao ni ya ushirikiano, ikitegemea taasisi za utafiti za ndani badala ya kuanzisha ofisi zao wenyewe.


Kikao hicho kilihudhuriwa pia na  Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba (Mb), Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango, ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato - TRA, Mhe. Mcha Hassan Mcha, Kamishna wa Walipakodi Wakubwa -TRA, Bw. Edmund Kawamala, Mkurugenzi wa Kituo cha Ubunifu wa ACET, Bw. Rob Floyd, Mratibu wa Uhamasishaji wa ACET, Bw. Tumna Tshimanga, Meneja Mawasiliano wa ACET, Bi. Belinda Ayamgha, na Mchumi wa ACET, Bw. George Awuah.








No comments