Zaidi ya sh. trilioni-4.6 zimetolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu-HESLB
Zaidi ya shilingi trilioni-4.6 zimetolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu-HESLB, ikiwa ni asilimia 60 ya fedha zote zilizowahi kutolewa na bodi hiyo tangu kuanzishwa kwake takriban miaka 22 iliyopita.
Mafanikio hayo yametangazwa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, wakati akizungumza na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) katika mkutano ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Dkt. Kiwia, amesema tangu kuanzishwa kwa bodi hiyo, jumla ya shilingi trilioni-9 zimetolewa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, hatua inayolenga kupanua fursa za elimu kwa wanafunzi wenye uhitaji.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali imetenga bajeti ya shilingi trilioni 1.06 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi, kiasi kinachotarajiwa kuwanufaisha wanafunzi takribani 300,000 bajeti hiyo inatajwa kuwa ni rekodi mpya katika historia ya utoaji wa mikopo hiyo chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande mwingine, katika mwaka wa fedha 2025/2026, HESLB ilikuwa na bajeti ya shilingi bilioni-916.7, iliyowanufaisha wanafunzi 289,932, ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 imeongezeka kwa takriban asilimia 15.6 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Kuhusu urejeshaji wa mikopo hiyo, Dkt. Kiwia, amesema HESLB bado inadai takriban shilingi bilioni-800 kutoka kwa wanufaika wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi katika sekta isiyo rasmi, akisisitiza umuhimu wa urejeshaji wa mikopo ili kuwezesha fedha hizo kutumika tena kuwanufaisha wanafunzi wengine.

.jpeg)


Post a Comment