WAGONJWA 6,145 WA SIKO SELI WABAINIKA MKOANI PWANI-MKURANGA YAONGOZAA

Mkoa wa Pwani unakadiriwa kuwa na jumla ya wagonjwa wa Siko Seli 6,145, kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa kupitia mahudhurio ya kliniki kati ya Januari hadi Desemba 2024, huku Wilaya ya Mkuranga ikiongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wagonjwa.

Takwimu hiyo imebainika, agost 12,2025 wakati wa semina ya siku moja kwa waandishi wa habari kuhusu ugonjwa wa Siko Seli, iliyoandaliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikisha madaktari bingwa na wataalamu wa magonjwa ya damu. 

Dkt. Pius Muzzazzi, Daktari Bingwa wa Watoto na Magonjwa ya Damu kutoka Hospitali ya Rufaa ya Tumbii ameeleza  licha ya Dar es Salaam kuongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa Siko Seli, lakini kati ya wagonjwa wanaopata matibabu katika vituo vya afya vya mkoa huo, asilimia 10 hadi 15 wanatoka Mkoa wa Pwani.

Amesema Wilaya ya Mkuranga inaongoza kwa kuwa na wagonjwa 1,444, Kibaha Mjini (1,290), Bagamoyo (1,078), Rufiji (582), Kibiti (541), Kisarawe (510), Chalinze (340), Kibaha Vijijini (305) na Mafia (155). 

Nae Mratibu wa Huduma za Siko Seli kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Asteria Mpoto, ameeleza semina hiyo imelenga kuwajengea uwezo viongozi wa dini, walimu, waandishi wa habari na makundi mengine ya jamii ili wawe mabalozi wa kutoa elimu sahihi kuhusu ugonjwa huo, dalili zake na namna ya kukabiliana nao.

Awali, akiwasilisha mada kuhusu ugonjwa huo, Dkt. Jamila Makame, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu kutoka Hospitali ya Amana, ameeleza kuwa ugonjwa huo ni wa kurithi unaosababishwa na vinasaba kutoka kwa wazazi wote wawili na unaweza kudhibitiwa iwapo utagunduliwa mapema na kuzingatia ushauri wa kitaalamu. 

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, mikoa inayoongoza kwa idadi ya wagonjwa wa Siko Seli nchini ni Dar es Salaam, ikifuatiwa na mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kigoma.

No comments