MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA (DCEA), YAKAMATA ZAIDI Kg.10 ZA DAWA ZA KULEVYA
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imesema kati ya mwezi Septemba na Oktoba 2025, imekamata jumla ya kilogramu 10,763.94 za aina mbalimbali za dawa za kulevya, pamoja na kilogramu 6,007 na lita 153 za kemikali bashirifu katika operesheni zilizofanyika katika maeneo mbalimbali nchini na Jumla ya watuhumiwa 89 walikamatwa kuhusiana na uhalifu huo.
Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es salaam Kamishina wa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya Aretas Lyimo amesema katika Eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, zilikamatwa dawa ya kulevya aina ya mirungi iliyokaushwa na kufungwa kama viungo (spices) yenye uzito wa kilogramu 40.32. Dawa hizo zilikuwa kwenye paketi 80 zenye maandishi "dry basil leaves", na zilikuwa tayari kusafirishwa kwenda Canada na Italy.
Aidha Kamishina Lyimo amesema Watuhumiwa waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo ni Yusuphu S. Kibaha (35) na Mohamed H. Ramadhan (41) na kuongeza kuwa taarifa za kiuchunguzi zimebainisha kwamba, dawa hizo za kulevya zilingizwa nchini kwa njia ya kificho kutokea nchi jirani na zilitumwa kupitia makampuni ya usafirishaji.
Sambamba na hayo, DCEA imesema imebaini kuwepo na mtandao wa usafirishaji wa dawa za kulevya aina ya mirungi, ambao hutumia bodaboda na kujenga mahusiano ya karibu na mawakala wa kampuni za usafirishaji nchini Tanzania ili kurahisisha usafirishaji wa dawa za kulevya bila kutiliwa shaka.
Katika operesheni nyingine iliyofanyika eneo la Mlalakuwa, wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam, watuhumiwa Bright A. Malisa (26), Humphrey G. Safari (26), Novatus A. Kileo (26) na Chriss P. Mandoza (26) walikamatwa wakitengeneza biskuti za bangi kwa ajili ya house party ya wanafunzi wa vyuo vikuu.




Post a Comment