WATOTO 9 WAFANYIWA UPASUAJI WA MOYO KWA MAFANIKIO JKCI
Watoto tisa wenye matatizo ya moyo ya
kuzaliwa nayo wamefanyiwa upasuaji wa moyo kwa mafanikio kwenye kambi maalumu
ya matibabu ya siku mbili iliyomalizika hivi karibuni katika Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Upasuaji huo umefanywa na wataalamu wa magonjwa ya
moyo kwa watoto JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Save a
Child’s Heart (SACH) la nchini Israel.
Akizungumza na waandishi wa habari Daktari Bingwa wa
Magonjwa ya Moyo kwa watoto, Stella Mongela alisema upasuaji huo ulifanyika kwa
njia ya tundu dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab ambao ni maabara maalumu
inayotumia mionzi kutambua na kutibu magonjwa ya moyo.
“Kambi hii imeokoa maisha ya watoto na kupunguza idadi
ya wagonjwa wanaosubiri upasuaji. Tumetoa huduma kwa watoto wenye matundu
kwenye moyo na wale wenye mishipa ya damu iliyoziba. Upasuaji huu mdogo
unawasaidia kuepuka upasuaji mkubwa wa kufungua kifua”, alisema Dkt. Stella.
Aliongeza kuwa miaka ya nyuma watoto wenye matatizo
hayo walikuwa wakipelekwa Israel kwa matibabu, lakini sasa huduma hizo
zinatolewa nchini kutokana na ujuzi na uzoefu mkubwa wa wataalamu wa JKCI.
“Upasuaji wa tundu dogo humsaidia mtoto kulazwa kwa
muda mfupi, kupona haraka na kurejea nyumbani akiwa na afya njema, hivyo
kupunguza gharama na usumbufu kwa familia”, alifafanua Dkt. Stella.
Dkt. Stella alisema watoto tisa waliowafanyia upasuaji
wa moyo wanaendelea vizuri na kuna ambao wameruhusiwa kurudi nyumbani.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa
watoto kutoka Shirika la SACH Assa Sagi alisema ameshuhudia maendeleo makubwa
katika utoaji wa huduma za moyo nchini.
“Nimeona jinsi madaktari wa JKCI walivyopata ujuzi na
uzoefu mkubwa. Sina haja tena kuja na timu nzima, kwani sasa huduma hizi
zinatolewa kwa ubora wa hali ya juu na madaktari wazawa”, alisema Dkt.
Sagi.
Dkt. Sagi aliongeza kuwa ushirikiano wa muda mrefu
kati ya Israel na Tanzania umeleta matunda chanya katika kubadilishana ujuzi na
teknolojia, hivyo kukuza sekta ya afya nchini.
Kwa upande wa wazazi ambao watoto wao wamefanyiwa
upasuaji kupitia kambi hiyo walishukuru kwa huduma bora zilizotolewa na
wataalamu wa JKCI na SACH zilizookoa maisha ya mtoto wao na wamefarijika kuona
huduma hizo zinapatikana hapa nchini bila kulazimika kwenda nje.
“Wazazi wenzangu wenye watoto wenye matatizo ya moyo,
msiwaache nyumbani. Waleteni JKCI wapate huduma mapema ili kuepuka kupata
changamoto kubwa zaidi”, alisema Mariam Rashid.
“Tulikuwa tunaishi kwa hofu, lakini sasa tumeona
matumaini mapya. Tunawashukuru JKCI na SACH kwa moyo wa huruma na kazi nzuri
wanayoifanya kwa watoto wetu”, alisema Abdallah Rashid.


Post a Comment