WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII DKT. KIJAJI AWATAKA WATUMISHI KUZINGATIA UTU WA MTANZANIA
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Ashatu Kijaji (Mb), amewataka watumishi wa wizara na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kuhakikisha wanazingatia maslahi na utu wa Mtanzania wanapotoa huduma kwa wananchi.
Dk. Kijaji ameyasema hayo jijini Dodoma mara baada ya kuripoti kazini na kufanya mazungumzo na menejimenti ya wizara, muda mfupi baada ya kuapishwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Amesema ni muhimu watumishi kufanya kazi kwa kuzingatia utu na maslahi ya wananchi ili kuhakikisha wanapata huduma bora na maendeleo wanayostahili.
Amefafanua kuwa Ilani ya CCM imeweka mkazo katika ustawi wa watu, na ustawi huo hauwezi kupatikana endapo changamoto kama wanyamapori waharibifu hazitatatuliwa.
Ameongeza kuwa falsafa ya Kazi na Utu ya Mhe. Rais inahitaji mtumishi kumweka mwananchi mbele: “unapomhudumia mtu, jiulize ungependa kuhudumiwa vivyo hivyo? Huo ndio msingi wa kazi yetu.” amesema Dk. Kijaji
Waziri Kijaji pia ametoa wito kwa watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na mshikamano ili kutimiza ndoto za Watanzania kupitia sekta za uhifadhi, maliasili na utalii.
Aidha, amewapongeza kwa kazi wanayoifanya na kuhimiza kuendeleza ushirikiano ili kufikia malengo ya wizara.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mhe. Hamad Hassan Chande ameishukuru menejimenti na watumishi kwa mapokezi mazuri na kusisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa kuzingatia utu.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Hassan Abbas, ameahidi kutoa ushirikiano kwa uongozi mpya ili kufanikisha malengo ya wizara na serikali, hususan katika kuhudumia wananchi na kutangaza vivutio vya utalii.
Awali, Waziri Dk. Kijaji alikagua gwaride maalum lililoandaliwa na Jeshi la Uhifadhi (JU) akiongozwa na Katibu Mkuu, Dk. Abbas.
.jpeg)
.jpeg)



.jpeg)

Post a Comment