WAHITIMU WAHIMIZWA KUTUMIA ELIMU KWA MAENDELEO
CHUO Kikuu Cha Dar es Salaam kimemtunuku Digrii ya Heshima ya Udaktari wa Fasihi na Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam Mwasisi na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Clementina, Dkt. Maria Josephine Kamm, kutokana na mchango wake mkubwa katika sekta ya elimu nchini.
Dkt. Kamm ametunukiwa Digrii hiyo leo Novemba 18, 2025, wakati wa mahafali ya 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) yaliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City.
Akihutubia maelfu ya wahitimu na wageni waalikwa, Dkt. Kamm amesema kumuelimisha msichana ni hatua muhimu katika kubadili sio tu maisha ya mtu mmoja, bali pia jamii nzima kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Amehimiza jamii kutokumkatia tamaa mtoto wa kike, badala yake kuhakikisha anapata elimu bora itakayomwezesha kujikomboa na kuchangia katika ujenzi wa jamii mpya.
Amesema anaamini elimu inapaswa kuwa ya vitendo na inayomuandaa kijana sio tu kufaulu mitihani, bali pia kuishi maisha yenye heshima, kutatua changamoto na kuwa na manufaa katika jamii.
Aidha, aliwataka wahitimu kutokata tamaa pindi wanapokutana na vikwazo katika safari yao ya kujifunza na kutafuta mafanikio.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Anangisye wakati akitoa hotuba yake, amesema zaidi ya mitaala 250 imepitiwa na inatarajiwa kuwasilishwa kwa TCU kwaajili ya kupitishwa, ambapo takribani mitaala 242 ya ngazi ya Shahada ya Awali na Uzamili tayari imewasilishwa.
Amesema Chuo kimewezesha utambuzi wa zaidi ya bunifu 120 na usajili wa kampuni changa 39, kama sehemu ya juhudi za kukuza ubunifu na ujasiriamali.
Kuhusu Ubunifu Prof. Anangisye amesema kuwa Chuo kimetoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanafunzi 569, wakiwemo wanafunzi 65 wenye ulemavu, ikiwa ni hatua ya kujenga uwezo jumuishi kwa maendeleo endelevu.



.jpeg)
Post a Comment