AFISA MAENDELEO KIKAANGONI UPOTEVU WA MIL. 516

Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Mhe. Reuben Kwagilwa, ameagiza kurejeshwa Halmashauri ya Masasi aliyekuwa Afisa Maendeleo wa halmashauri hiyo ili kujibu tuhuma za kutokujulikana zilipo shilingi milioni 516 zilizodaiwa kugawanywa kwa vikundi visivyokuwa na kumbukumbu.


Mhe. Kwagilwa ametoa maelekezo hayo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, OWM–TAMISEMI, Mhe. Profesa Riziki Shemdoe, wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Mtwara, ambapo amekagua miradi ya shule na barabara pamoja na kufuatilia matumizi ya fedha za Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


“Nitumie fursa hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, kuwaonya na kuwakumbusha watumishi wa halmashauri nchi nzima kuwa na nidhamu. Hatutaruhusu fedha za umma kuguswa, kudokolewa au kutumika nje ya mipango iliyokubaliwa,” amesema Mhe. Kwagilwa.


Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mtwara kuwaweka ndani na kuwahoji Mhandisi wa Ujenzi pamoja na Mweka Hazina wa halmashauri kwa madai ya kutumia fedha za umma bila kufuata miongozo iliyowekwa.


Aidha, akisisitiza uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za umma, Mhe. Kwagilwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, kuzielekeza taasisi za uchunguzi kufanya uchunguzi katika Halmashauri ya Nanyamba kuhusu fedha zilizochukuliwa na Kikundi cha Kimbilio Youth Group, na iwapo itabainika fedha hizo hazikupitia taratibu zilizopangwa, hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.

No comments