AWESOME: BWAWA LA KIDUNDA KUZALISHA MAJI LITA BILIONI 20 KWA SIKU
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema Bwawa la Maji la Kidunda linatarajia kuwa na uwezo wa kuzalisha hadi lita bilioni 20 za maji kwa siku kwa ajili ya huduma ya maji safi na salama. Amesema mradi huo utatoa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya upungufu wa maji inayolikabili Jiji la Dar es Salaam na mikoa ya Pwani, hususan inayosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Waziri Aweso ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda mkoani Morogoro, mradi wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 329 ambao unasimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).
Amesema dunia kwa sasa inakabiliwa na changamoto ya ukame inayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, hali ambayo pia imeanza kuiathiri Tanzania. Kutokana na hali hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliielekeza Wizara ya Maji kuchukua hatua za haraka na za muda mrefu ili kukabiliana na changamoto hiyo.
“Wizara ya Maji tuliweka mkakati wa muda mfupi jijini Dar es Salaam kwa kuchimba visima vitano vilivyogharimu takribani Shilingi bilioni 23.6, sanjari na mkakati wa muda mrefu wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda mkoani Morogoro pamoja na mpango wa kutumia maji ya Mto Rufiji mkoani Pwani ili kuongeza uzalishaji wa maji,” Waziri Aweso amefafanua.
Amesema kwa sasa mahitaji ya maji kwa Jiji la Dar es Salaam ni takribani lita milioni 534 kwa siku, ilihali changamoto ya ukame ikiathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma ya maji.
Kutokana na hali hiyo Serikali imetoa kipaumbele kukamilisha ujenzi wa Bwawa la Kidunda, ambao hadi sasa umefikia asilimia 40 ya utekelezaji na utakuwa ni suluhisho la kudumu kwa huduma ya maji kwa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.
Waziri Aweso ameongeza kuwa kazi nyingi za kiufundi za mradi huo zimekamilika, na kazi kubwa iliyosalia ni kukamilisha ujenzi wa mageti ya bwawa. Amesisitiza kuwa ifikapo mwezi Aprili, 2026 maji ya Mto Ruvu yataanza kuingia kwenye bwawa hilo.
Katika hatua nyingine, Waziri Aweso amesema Serikali itaendelea na mkakati wa kujenga mabwawa ya kuhifadhi maji katika maeneo mbalimbali nchini ili kuvuna maji ya mvua.

Post a Comment