MAAFISA UHAMIAJI WAHUKUMIWA KUNYONGWA
Mahakama Kuu ya Tanzania imewahukumu kunyongwa hadi kufa maafisa watatu wa Idara ya Uhamiaji, Fredrick Kyomo, Joachim Trathizius na Mabruki Hatibu, baada ya kuwakuta na hatia ya kumuua Enos Elias, mkazi wa Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, waliyemdhania kuwa si raia wa Tanzania.
Kulingana na The Citizen, hukumu hiyo imetolewa Jumatatu, Desemba 15, 2025, na Jaji wa Mahakama Kuu, Augustine Rwizile, aliyesema ushahidi uliowasilishwa mbele ya mahakama umethibitisha pasipo shaka kuwa mauaji hayo yalifanywa na washtakiwa hao watatu pekee bila kuhusisha mtu au kundi lingine lolote.
Akisoma hukumu, Jaji Rwizile amesema ushahidi unaonesha wazi kuwa washtakiwa walimkamata marehemu, wakamshambulia na baadaye kumpeleka katika eneo lisilojulikana ambako alikutwa akiwa amefariki dunia, hali inayothibitisha kuwa walitenda kosa hilo kwa nia ovu.
“Kwa kuzingatia ushahidi unaoonesha namna walivyomkamata, kumpiga na hatimaye kumpeleka katika eneo lisilojulikana ambako alikutwa akiwa amekufa, vitendo hivyo vinatosha kuthibitisha kuwa washtakiwa walitekeleza kosa hilo kwa makusudi,” alisema Jaji Rwizile.
Kwa mujibu wa ushahidi wa mahakama, Enos Elias alikamatwa na maafisa hao wa uhamiaji katika kizuizi cha Kihomoka, Wilaya ya Kakonko, Oktoba 27, 2023, kisha kupelekwa katika ofisi za uhamiaji kwa mahojiano.
Akiwa kizuizini, marehemu aliwasiliana na ndugu zake na kuwaomba wamletee kitambulisho chake cha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kama uthibitisho wa uraia wake. Hata hivyo, ndugu hao walipofika ofisini kufuatilia suala hilo, waliambiwa kuwa Elias alikuwa tayari ameachiwa huru Oktoba 28, 2023.
Baada ya hapo, marehemu hakupatikana tena, simu yake ilikuwa haipatikani, hadi mwili wake ulipogunduliwa Oktoba 29, 2023, na kuzikwa bila uwepo wa ndugu wala familia yake.

Post a Comment