DC. GONDWE MGENI RASMI KUAGWA AFISA WA MAGEREZA SINGIDA


Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhe. Godwin Gondwe, amewataka maafisa na askari wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Singida kuiga mfano wa utumishi uliotukuka wa  aliyekuwa Mnadhimu wa Magereza mkoa wa Singida, Kamishina Msaidizi wa Magereza (ACP) Felix Mwakyusa, kwa kujitoa kikamilifu katika kazi  kwa manufaa ya taifa.


Mhe. Gondwe aliyasema hayo Disemba 19, 2025  alipokuwa akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, katika hafla ya kumuaga rasmi ACP Felix Mwakyusa iliyofanyika jioni katika Ukumbi wa Aqua Conference Hall, Manispaa ya Singida.


Gondwe alisema kuwa kustaafu sio mwisho wa kufanya kazi bali ni kubadili mfumo wa maisha, akisisitiza kuwa taifa bado linaweza kumhitaji mstaafu huyo muda wowote atakapohitajika kutokana na uzoefu na mchango wake mkubwa alioutoa katika Jeshi la Magereza kwa kipindi cha miaka 35.


Mhe. Gondwe aliongeza kuwa ACP Mwakyusa amekuwa mtumishi mwenye unyenyekevu na upendo mkubwa kwa walio chini yake, akimtaka aendelee kudumisha sifa hizo hata katika jamii anayokwenda kuishi baada ya kustaafu.


Kwa upande wake, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) Khabu Juma Semzono alimpongeza ACP  Mwakyusa kwa utendaji kazi wake uliotukuka, akisema amekuwa msikivu na mtekelezaji mzuri wa majukumu aliyokuwa akimpa kama msaidizi wake.

No comments