HALI YA NCHI NI SHWARI - JESHI LA POLISI

Jeshi la Polisi nchini Tanzania linasema mpaka sasa (majira ya mchana) hali ya usalama wa nchi ni nzuri na vyombo vya ulinzi vinaendelea kuimarisha usalama katika maeneo mbalimbali.

Katika taarifa iliyotolewa na Msemaji wa jeshi hilo, David Misime amesema hali inaendelea vyema na wanawahakikishia wananchi usalama wao pamoja na mali zao.

Aidha, Misime ametoa wito kwa wananchi kupuuza picha na picha mjongeo zinazosambaa kwenye ya mitandao ya kijamii zikionyesha kuwa maandamano yameanza katika baadhi ya maeneo nchini.

Misime amesema, “kuna watu wanatuma mitandaoni picha za tarehe 29,30,31 Oktoba, tunawahimiza kupuuza picha hizo kwani taarifa zake si sahihi.”

Maandamano ya amani yaliyopangwa kufanyika siku ya leo yalipigwa marufuku na mamlaka za Serikali yakidaiwa kuwa hayakukidhi matakwa ya kisheria.

Taarifa katika miji mikuu nchini Tanzania, zinaeleza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea na doria katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Hata hivyo, mpaka sasa BBC haijashuhudia kundi lolote linalodaiwa kuwa ni la waandamanaji katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam na linaendelea kuhakika taarifa za kuwepo kwa maandamano katika maeneo mengine ya nchi hiyo.

No comments