MANISPAA YA KIBAHA YATENGA MAMILIONI YA FEDHA UJENZI WA MADARASA NA MADAWATI SHULE ZA SEKONDARI
HALMASHAURI ya Manispaa ya Kibaha imetenga mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu katika shule za sekondari, zikiwemo sh.milioni 900 kwa ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa na sh. milioni 400 kwa ununuzi wa madawati.
Akizungumza na waandishi wa habari Disemba 10, 2025, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo, Dkt. Mawazo Nicas, ameeleza wamejipanga kikamilifu kuimarisha na kuboresha sekta ya elimu ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi.
Amesema wanafunzi 6,000 wamefaulu mtihani wa darasa la saba mwaka huu, sawa na asilimia 100, ikilinganishwa na wanafunzi 3,050 waliofaulu mwaka uliopita, hali inayoonesha ongezeko kubwa la ufaulu.
Dkt Nicas ameongeza kuwa, ujenzi wa madarasa mapya unatarajiwa kukamilika ndani ya siku 60 na mzabuni tayari amepatiwa kazi ya kuyatengeneza ili ifikapo mwaka ujao yawe tayari kwa matumizi ya wanafunzi.
Vilevile ameitaka jamii pamoja na watendaji wa elimu kuhakikisha watoto wote waliofikia umri wa kuandikishwa katika darasa la awali na darasa la kwanza wanasajiliwa kwa mujibu wa taratibu.



Post a Comment