KASEKENYA AAGIZA BARABARA RUNGWE ZIKAMILIKE KWA WAKATI
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Mbeya kushirikiana kwa karibu na Mhandisi mshauri, TECU, katika kumsimamia mkandarasi CRBC anayetekeleza ujenzi wa barabara za Mbaka–Kibanja (km 20.7) na Katumba–Lupaso (km 35.3), ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati uliopangwa.
Mhandisi Kasekenya ametoa agizo hilo leo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa ujenzi wa barabara ya Katumba–Mbambo–Tukuyu yenye urefu wa kilomita 79.4, wilayani Rungwe.
“Hakikisheni ujenzi unatekelezwa kwa kuzingatia viwango vilivyokubaliwa, na barabara haifungwi wakati wote wa ujenzi ili shughuli za usafiri na uchukuzi zisiathirike,” amesisitiza Mhandisi Kasekenya.
Aidha, amesisitiza kuwa ujenzi wa barabara zote mbili za Mbaka–Kibanja na Katumba–Lupaso utekelezwe kwa wakati mmoja ili zikamilike kwa pamoja na kuleta tija kwa wananchi wa Wilaya ya Rungwe.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Sulemani Bishanga, amesema ujenzi wa barabara hizo tayari umeanza na umefikia asilimia 4.6, na unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 36.
Mbunge wa Busokelo, Lutengano Mwalwiba, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuimarisha miundombinu ya barabara wilayani Rungwe, akibainisha kuwa miradi hiyo imetoa ajira kwa vijana na kusaidia kukuza ujuzi wao.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jafari Haniu, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuelekeza miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo, na kumhakikishia Mkandarasi ushirikiano wa kutosha
Mkandarasi wa mradi huo, Kampuni ya CRBC, ameahidi kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia mkataba ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati, pamoja na kupunguza adha kwa watumiaji wa barabara hizo wakati wa utekelezaji wa ujenzi.
Ujenzi wa barabara za Mbaka–Kibanja (km 20.7) na Katumba–Lupaso (km 35.3) ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuifungua Wilaya ya Rungwe kwa mtandao wa barabara za lami. Tayari ujenzi wa barabara za Lupaso–Bujesi (km 10), Bujesi–Mbaka (km 12.6) na Kibanja–Tukuyu (km 7) umekamilika.

Post a Comment