TANZANIA NA UTURUKI KUIMARISHA UWEZESHAJI WA VIJANA NA WANAWAKE

 

Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuanzisha makubaliano yatakayowezesha vijana wa Tanzania kunufaika na fursa za mafunzo, uzoefu wa biashara na kuunganishwa na vijana wenzao kupitia Jukwaa la Young MÜSIAD ili kukuza mtandao wa biashara, ujuzi na kuandaa rasilimaliwatu itakayoimarisha biashara na uwekezaji kati ya nchi hizi mbili.


Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu wakati wa ziara ya kikazi nchini Uturuki Desemba 18, 2025. Wakati wa ziara Katibu Mkuu alifanya mazungumzo na Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wamiliki wa Viwanda (MÜSIAD) na Shirika la Women and Democracy Foundation (KADEM) za nchini Uturuki.


Kupitia mazungumzo na MÜSIAD, Viongozi hao walijadili fursa za ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki kwenye maeneo ya uwezeshaji wa vijana kiuchumi kupitia programu za uanagenzi, ubunifu, teknolojia na ziara za mafunzo (exchange programs) ili kuwezesha vijana kunufaika na ujuzi wa kimataifa kwenye sekta ya biashara.


Dkt. John amesema hatua hiyo inazingatia ukweli kwamba Tanzania na Uturuki ni washirika wazuri kwenye sekta ya biashara na nchi hizi mbili zina dhamira ya kukuza ushirikiano huo ili kuchochea urari wa biashara na manufaa ya kiuchumi yatokanayo na sekta hiyo. 


Dkt. Jingu amesema katika kufanyia kazi masuala muhimu yaliyokubalika kwenye kikao hicho, Tanzania na Uturuki zimeanza majadiliano yatakayowezesha utekelezaji wa makubaliano hayo na Ubalozi wa Tanzania nchini Uturuki utaendelea kuratibu zoezi hilo kwa kushirikiana na sekta husika.


Jumuiya ya MÜSİAD ni mahiri nchini Uturuki na duniani yenye uzoefu wa zaidi ya miaka 35 katika sekta ya biashara na uchumi, ikiwa na wanachama zaidi ya 60,000 kwenye sekta 25, hivyo, makubaliano hayo yatachochea maendeleo ya vijana kwenye sekta ya biashara. 


Kwa upande wa Shirika la KADEM mazungumzo hayo yalijikita katika kuimarisha ushirikiano wenye tija kwenye sekta ya maendeleo ya wanawake kupitia shughuli zinazotekelezwa na Shirika hilo ikiwemo mafunzo stadi ya biashara na ajira, haki za wanawake na kuhamasisha uwakilishi na ushiriki wao.

No comments