MAPYA YAIBUKA KIFO CHA JENISTA, ALIKUWA NA TATIZO LA KUANGUKA GHAFLA
Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, ameeleza hadharani kuwa marehemu Jenista Mhagama alikuwa akikabiliwa na changamoto ya kuanguka ghafla mara kwa mara katika kipindi cha hivi karibuni.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu Itega, Jijini Dodoma, ambapo viongozi na waombolezaji mbalimbali wameendelea kufika kutoa pole, Mchengerwa amesema kuwa marehemu Jenista aliwahi kumueleza binafsi kuhusu matatizo hayo.
“Tulikuwa na mawasiliano mengi sana. Mimi nafahamu kwamba wakati wa uchaguzi alipata changamoto ya kuanguka pia. Baada ya matokeo kutangazwa alipata changamoto hii na alianguka ghafla. Alinifahamisha yeye mwenyewe, na hata wakati Mheshimiwa Rais anaapishwa alinieleza kwamba alipata changamoto ya kuanguka ghafla,” amesema Waziri Mchengerwa.
Ameongeza kuwa hata siku za karibuni, marehemu alipatwa tena na tukio kama hilo, jambo ambalo anaamini linatoa funzo kwa Watanzania wote kuhusu umuhimu wa kuchukua tahadhari za kiafya.
“Pengine unaweza kuwa na tatizo la moyo hujui, lakini zipo ishara. Unapoona ishara hizo ni vyema kwenda kufanya vipimo kujua hali yako, kwa sababu unaweza kuwa mzima leo lakini ghafla ikatokea changamoto ya kiafya,” amesema.

Post a Comment