MSIGWA AZITAKA SEKTA BINAFSI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KATIKA KUWEKEZA KWENYE SEKTA ZA WIZARA YA HABARI UTAMADUNI SANAA NA MICHEZO


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Msigwa ametoa wito kwa Sekta Binafsi kushirikiana na Serikali katika kuwekeza kwenye sekta za wizara hiyo.


Msigwa ameyasema hayo tarehe 10, Desemba 2025 jijini Dodoma wakati alipofungua Mafunzo kwa Menejimenti na Wakuu wa Taasisi wa wizara hiyo kuhusu Ubia kati ya Sekta binafsi na Serikali (PPP) yenye lengo la kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya wizara na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya maendeleo ya 2050.

Ameongeza kuwa, ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi zitasaidia kuongeza na kuboresha miundombinu ya Michezo, ambapo Serikali inaendelea na ujenzi wa viwanja mbalimbali nchini.

"Tutajenga viwanja vya mazoezi na michezo Dar es Salaam, Arusha, na Dodoma, na tunajiandaa katika programu kubwa ya ujenzi wa vituo vya michezo na burudani nchi nzima lakini serikali haiwezi kufanya mambo yote peke yake lazima tushirikiane " alisema Msigwa

Vilevile amesema kuwa, ushiriki wa sekta binafsi ni hitaji la kisera ili kusaidia wananchi kunufaika na uchumi kupitia sekta ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mafunzo mengine yaliyotolewa ni Sheria ya Mikopo ya Dhamana na Misaada ya Serikali na Takwimu rasmi za Serikali.





No comments