SERIKALI YASISITIZA UBUNIFU KATIKA UNUNUZI NA UGAVI


Serikali imewataka wataalam wa ununuzi na ugavi nchini kuongeza ubunifu, uongozi bora na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza ufanisi, uwazi na tija katika matumizi ya fedha za umma.


Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati akifungua Kongamano la 16 la Wataalam wa Ununuzi na Ugavi lenye kaulimbiu ya “Kukuza Wataalam wa Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi watakaojiimarisha katika Ujuzi wa Uongozi na Ubunifu” lililoandaliwa na Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), jijini Arusha.


Mhe. Mhandisi Munde, alisema Serikali imejipanga kuimarisha usimamizi wa manunuzi kupitia Mfumo wa Kidigitali wa Ununuzi wa Umma, maarufu kama NeST, ili kupunguza gharama za ununuzi, kuongeza uwazi, kasi ya utekelezaji, kuzingatia bei ya soko, na kuleta tija kwa Taifa.


“Serikali imeelekeza shughuli zote za ununuzi zifanyike kupitia Mfumo wa NeST ili kuongeza uwazi, kupunguza gharama, na kuhakikisha thamani halisi ya fedha inapatikana katika miradi ya maendeleo,” alisema Mhe. Mhandisi Munde.


Aliongeza kuwa, utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unategemea sana weledi na uadilifu wa wataalam wa ununuzi na ugavi, hivyo Serikali itahakikisha Sheria na Kanuni za Ununuzi wa Umma zinazingatiwa kikamilifu katika ngazi zote za Serikali na sekta binafsi.


Aidha, Mhe. Mhandisi Munde aliiagiza PSPTB kushirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ili kuhakikisha shughuli zote za ununuzi na ugavi nchini zinafanywa na wataalam waliosajiliwa rasmi na PSPTB.


“Waajiri wote nchini wahakikishe wanawatumia wataalam waliosajiliwa na PSPTB kama inavyoelekezwa na Sheria Na. 23 ya Mwaka 2007 ilivyoanzisha PSPTB, hii italeta weledi, uwajibikaji na kuepusha upotevu wa fedha za umma,” alisisitiza Mhe. Mhandisi Munde.

No comments