SIMBACHAWENE AAPISHWA KUWA MWENYEKITI WA TUME VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma Mhe. Dkt. Juliana Masabo, Desemba 15, 2025 amemuapisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene (Mb), kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Idara ya Uhamiaji.
Katika hafla hiyo, Mhe. Masabo pia amemuapisha Kamishna wa Utawala na Rasilimali Watu wa Jeshi la Magereza, CP. Ahmad Mwen-dadi, pamoja na Kamishna wa Uhamiaji, DCI Joseph Mtenga, kuwa Wajumbe wa Tume hiyo. Zoezi la uapisho huo limefanyika katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo Jumuishi cha Utoaji wa Haki, jijini Dodoma.
Akizungumza mara baada ya kuwaapisha wajumbe hao, Mhe. Jaji Dkt. Masabo amewasisitiza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, weledi na kwa kuzingatia misingi ya haki kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo. Aidha, amepongeza ushirikiano uliopo kati ya vyombo vya ulinzi na usalama chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Mahakama ya Tanzania.
Vilevile, Mhe. Jaji Masabo amelipongeza Jeshi la Magereza kwa juhudi za kuboresha miundombinu ya magereza, hususani katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, pamoja na matumizi ya Mahakama mtandao, akibainisha kuwa mfumo huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuharakisha mchakato wa utoaji wa haki katika Mahakama zetu hapa nchini.
“Katika utekelezaji wa majukumu yenu, niwasihi mtende haki bila upendeleo wala uonevu, mkizingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo,” alisisitiza Mhe. Jaji Masabo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mhe. George Simbachawene (Mb), amemhakikishia Mhe. Jaji Masabo kuwa Tume itaendelea kusimamia sheria na kutenda haki bila kumuonea mtu yeyote. Aidha, amesisitiza kuendeleza ushirikiano baina ya vyombo vya ulinzi na usalama anavyoviongoza na Mahakama ya Tanzania, akieleza kuwa Jeshi la Magereza ni sehemu muhimu ya mnyororo wa haki jinai.
Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa Tume itasimamia na kuendeleza juhudi za kuboresha miundombinu ya Magereza ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Post a Comment