UWEKEZAJI BAGAMOYO WAFIKIA PAZURI, PROFESA KITILA ASHIRIKI MAKABIDHIANO
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb,) leo Disemba 30 ameshiriki hafla ya Makabidhiano ya hati kwa wawekezaji katika eneo Maalumu la Uwekezaji la Bagamoyo.
Katika hafla hiyo, Mhe Prof. Mkumbo pia ametoa taarifa ya uwekezaji kwa mwaka 2025 ambapo ameonesha kuwepo kwa ongezeko kubwa katika miradi ya uwekezaji inayosajiliwa sambamba na ongezeko la mtaji wa kutoka nje (FDIs).
“Katika kipindi cha miaka minne, Tanzania imeshuhudia mabadiliko makubwa ya kitakwimu yanayoashiria kuimarika kwa imani ya wawekezaji duniani” alisema na kutaja takwimu hizo kuwa ni pamoja na;
i. Usajili wa Miradi: idadi ya miradi imeongezeka kutoka miradi 252 mwaka 2021 hadi kufikia miradi 915 mwaka 2025, likiwa ni ongezeko la zaidi ya mara tatu.
ii. Mtaji wa Kigeni (FDI): Thamani ya mitaji kutoka nje imepanda kutoka Dola za Marekani Bilioni 3.7 mwaka 2021 hadi kufikia rekodi ya Dola Bilioni 10.95 mwaka 2025.
Mhe. Prof. Mkumbo amesema kuwa, Uwekezaji huo haujaishia kwenye namba tu, bali umegusa maisha ya Watanzania moja kwa moja kupitia uzalishaji wa ajira, ambapo ametanabaisha kuwa zaidi ya ajira mpya 161,678 zitazalishwa kupitia utekelezaji wa miradi hiyo.
Sekta za Viwanda (Manufacturing), Ujenzi na Usafirishaji zimekuwa kinara katika kuchochea ukuaji wa sekta ya uwekezaji nchini.
Uchambuzi wa taarifa ya Waziri unaashiria kuwa kasi hii inachochewa na mambo makuu matatu:
i. Uongozi Madhubuti: Jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kufungua nchi na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
ii. Sera Zinazotabirika: Uwepo wa sheria za kifedha na uwekezaji ambazo hazibadiliki hovyo, hali inayotoa uhakika kwa wawekezaji.
iii. Vivutio vya Kiuchumi: Kazi kubwa inayofanywa na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (TISEZA) katika kutoa vivutio vya kodi na kurahisisha huduma mahali pamoja (One-Stop Centre).
Post a Comment