WIZARA YA KATIBA NA SHERIA TANZANIA NA AFRIKA KUSINI ZAFANYA MAZUNGUMZO
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Sheria na Maendeleo ya Katiba wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Andries Nel, pembezoni mwa mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Sheria wa Umoja wa Afrika unaofanyika tarehe 16-17 Desemba, 2025 jijini Nairobi.
Katika kikao hicho, Mheshimiwa Andries Nel aliwasilisha salamu za pongezi kwa Mheshimiwa Dkt. Juma Zuberi Homera kufuatia kuteuliwa kwake kushika wadhifa wa Waziri wa Katiba na Sheria. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha na kuboresha ushirikiano wa kimataifa, hususani katika masuala ya Sheria na Haki.
Vilevile, Mhe. Andries Nel aliomba fursa ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria ya Tanzania, ikiwemo Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), kwa lengo la kujifunza uzoefu na uendeshaji wake ili kuboresha taasisi yake inayo fanya kazi sawa na RITA.
Katika mazungumzo hayo, Andries Nel alipongeza utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ( Mama Samia Legal Aid Campaign) inayotekelezwa na Wizara ya Katiba na Sheria akibainisha kuwa imekuwa chachu kubwa ya kukuza Haki na uwajibikaji nchini Tanzania na barani Afrika.
Sanjari na hilo alipongeza hatua iliyofikiwa na Tanzania katika makubaliano ya nchi za Afrika ya kutengeneza eneo huru la Biashara la Bara la Afrika kwa lengo la kuunda soko moja la pamoja barani Afrika kwa bidhaa na huduma.
Kwa upande wake, Dkt. Homera alimkaribisha Naibu Waziri wa Sheria wa Afrika Kusini kutembelea Tanzania ili kujifunza jinsi RITA inavyofanya kazi, kubadilishana uzoefu wa masuala ya Haki za Binadamu, Utawala Bora na Utawala wa Sheria, na kujionea fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini, ikiwemo uwekezaji katika kilimo, utalii na uhifadhi wa wanyama pori, viwanda, sekta ya madini pamoja na usafirishaji.

Post a Comment