KIWANDA CHA FORTUNE PAPER KILICHOPO MISUGUSUGU CHASIMAMISHWA KWA SIKU 7 KUFANYA MAREKEBISHO
WANANCHI wa Kata ya Misugusugu, Manispaa ya Kibaha, wamelalamikia uchafuzi mkubwa wa mazingira unaotokana na maji machafu yanayotiririshwa na baadhi ya viwanda, ikiwemo Kiwanda cha karatasi cha Fortune Paper, hali iliyolazimu Manispaa kusimamisha shughuli za kiwanda hicho ndani ya wiki moja kufuatia agizo la Meya wa Manispaa hiyo, Dkt. Nicas Mawazo.
Malalamiko hayo yametolewa wakati wa ziara ya Meya wa Manispaa ya Kibaha katika kata hiyo, ambapo wananchi walieleza kuwa maji yenye kemikali hutiririshwa kutoka viwandani hususan kipindi cha mvua, na kusababisha madhara ya kiafya ikiwemo kuwashwa miili na kuungua miguu.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Diwani wa Kata ya Misugusugu, Ally Simba, ameeleza changamoto ya maji taka kutoka viwandani imekuwa kubwa na kuathiri moja kwa moja makazi, mashamba na afya za wananchi.
Mkazi wa Misugusugu, Mataba Matiku, amesema maji machafu yanayotiririshwa na baadhi ya viwanda yamesababisha kuungua miguu yake, akiiomba Serikali kuchukua hatua madhubuti .
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Saeni, Edward Kitale, ametaja baadhi ya viwanda vinavyolalamikiwa kuwa ni pamoja na kiwanda cha sabuni, Kiwanda cha karatasi cha Fortune Paper pamoja na kiwanda cha misumali cha Vunjo.
Kutokana na malalamiko hayo, Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, amefanya ziara ya kushtukiza katika Kiwanda cha Fortune Paper na kuagiza kusimamishwa kwa shughuli zake kwa wiki moja baada ya kubainika kukiuka sheria za mazingira mara tatu licha ya kulipishwa faini.
Vilevile, ameitaka Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC )kwa kushirikiana na maofisa mazingira wa Manispaa ya Kibaha kufika katika viwanda ili kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wawekezaji na kutoa ufumbuzi wa haraka wa kudhibiti uchafuzi wa mazingira.
Ofisa Mazingira wa Manispaa ya Kibaha, Rahel Ulaya, amesema mwekezaji wa Kiwanda cha Fortune Paper hajazingatia masharti ya mazingira, hivyo kwa mujibu wa agizo la Meya, shughuli za kiwanda hicho zimesimamishwa kwa muda hadi pale watakapojenga mifumo ya kisasa ya kuchuja maji taka ili kuzuia madhara kwa wananchi.
Mmoja wa wahusika wa uwekezaji wa kiwanda cha Fortune alikiri kupewa onyo mara kadhaa, na ameahidi kufanya marekebisho ambayo amepewa maelekezo ndani ya siku saba.




Post a Comment