NAIBU WAZIRI HAMISI MWINJUMA AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI KITUO CHA AFYA MGAMBO

NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Muheza, Mhe. Hamis Mwinjuma (MwanaFA), amesema kuwekwa kwa jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Afya Mgambo kumemfanya "roho yake iwe baridi" baada ya kutimiza ahadi iliyosubiriwa kwa miaka 18 na wakazi wa Tarafa ya Amani.

Mradi huo wenye thamani ya Shilingi 645,282,482, unatarajiwa kuhudumia zaidi ya watu 39,000 na unapaswa kukamilika ndani ya miezi sita, ifikapo Mei 2026, chini ya mkandarasi kampuni ya CJ Engineering.
Akizungumza na mamia ya wananchi wa Kijiji cha Mgambo-Miembeni, Mhe. MwanaFA amesema uwekaji wa jiwe hilo utamfanya leo apate usingizi wa amani kwani alikuwa na uchungu na kero hiyo kiasi cha kuahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni 100 kutoka mfukoni mwake endapo Serikali isingeweka fedha kufikia Oktoba 29 mwaka huu.

"Mchakato wa Serikali una taratibu zake, na ndiyo maana tangu fedha ziletwe Septemba kulikuwa na ucheleweshwaji uliozua maswali kwa wananchi wakati wa kampeni. Niliahidi kuingia mfukoni kuanza ujenzi kama Serikali ingechelewa, lakini namshukuru Rais Dkt. Samia kwa kutoa fedha hizi na kuthibitisha kuwa Muheza tunasikilizwa," alisema MwanaFA.
MwanaFA amebainisha kuwa tangu Wilaya ya Muheza ianzishwe mwaka 1974, ilikuwa na kituo kimoja tu cha afya (Mkuzi), lakini katika uongozi wa Rais Samia, jimbo hilo limepata vituo vingine vinne ikiwemo Kwafungo (Mil. 500), Ubwari na sasa Mgambo, huku ujenzi wa Misozwe (Mil. 250) ukiwa njiani. 

Ili kuimarisha huduma hapo hapo, MwanaFA ametoa agizo kwa Mganga Mfawidhi kuhakikisha gari la wagonjwa (Ambulance) lenye namba STM 7850 linapaki katika Kituo cha Afya Mgambo ili kuhudumia wananchi mara moja. 
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Fani Mussa, amesema kituo hicho kitatoa huduma zote zikiwemo za upasuaji na kulaza wagonjwa, huku watumishi watano wakiwa tayari wameshafika na wengine wanne (akiwemo mtaalamu wa meno) wakitarajiwa Januari.
Mbunge huyo ametoa shukrani za pekee kwa familia ya Marehemu Zuber Mshuza na mkewe Asia Maneno, kwa kukubali kutoa eneo lao kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho, kitendo alichokiita ni cha kizalendo na kiungwana.

Mwenyekiti wa Halmashauri, Salimu Shechambo, na Katibu wa UVCCM Wilaya, Ajuaye Msigala (kwa niaba ya Katibu wa CCM), wamempongeza MwanaFA kwa kuwa na "Spidi ya 5G" ya maendeleo na kuwataka wananchi kuwa walinzi wa vifaa vya ujenzi ili mradi ukamilike kwa thamani ya fedha.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji, Ernest John, amesema Mbunge huyo amewavika nguo viongozi wa kata kwani mradi huo ulikuwa na ahadi nyingi zisizotekelezeka kwa miaka 18 iliyopita.

No comments