TRA YAPAMBANA VIKALI NA UKWEPAJI KODI, YAIMARISHA MIFUMO YA UKUSANYAJI


Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema TRA itaendelea kupambana na watu wote wanaojihusisha na vitendo vya ukwepaji wa kodi kwa kudhibiti mianya inayotumika kukwepa kodi.

Akihitimisha kikao cha tathmini ya utendaji kazi wa TRA kwa kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2025/2026 kilichofanyika kwa muda wa wiki moja kwenye ukumbi wa mikutano wa Kimataifa AICC jijini Arusha na kuisha mwishoni mwa wiki iliyopita, (09.01.2026) Kamishna Mkuu Mwenda alisema hawatawavumilia vitendo vyovyote vya ukwepaji wa kodi.

Alisema miongoni mwa hatua watakazochukua ni kuimarisha mipaka, kuzuia magendo na kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa jamii sambamba na elimu ya magendo. 

Sambamba na kupambana na wakwepaji kodi Kamishna Mkuu alisema wamejipanga kuongeza wigo wa kodi kwa kusajili walipakodi wapya wakiwemo wafanyabiashara ambao bado hawajaingia katika mifumo ya kulipa kodi.

Alisema TRA itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu kama ilivyo jadi yake kwa kuwasikiliza walipakodi, kuwezesha biashara zao na kutatua changamoto zinazowakabili. 

Aidha Bw. Mwenda aliwataka watumishi wa TRA kuendelea kufanya kazi kwa weledi na bidii ili kuweza kuleta matokeo chanya katika ukusanyaji wa Mapato ya Serikali kwa Nusu ya Pili ya Mwaka wa Fedha 2025/26.


Kamishna Mkuu Mwenda alisema kazi ya kukusanya kodi ni ya watumishi wote na siyo maafisa kodi pekee hivyo kila mtumishi wa TRA anapaswa kuhakikisha anatumia ubunifu, weledi na kuzingatia maadili ili kutimiza malengo ya TRA ya kukusanya Shilingi Trilioni 36.066 katika Mwaka wa Fedha 2025/26.

Alifafanua kua ni matumaini yake kuiona TRA inakusanya kodi kwa ufanisi na hatimaye kulifanya Taifa kujitegemea kupitia kodi zake.

Akizungumza kuhusu mikakati ya ukusanyaji kwa Nusu ya Pili ya Mwaka wa Fedha 2025/26 Kamishna Mkuu Mwenda amesema TRA imejidhatiti kuhakikisha inaendelea kutumia mifumo katika ukusanyaji wa kodi huku akiutaja mfumo wa IDRAS ambao utaanza rasmi Febuari 9, 2026.

Mbali na hayo, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia TRA watumishi wapya huku akitoa wito kwa viongozi kuwasimamia watumishi hao ili waweze kuleta tija katika utendaji wa majukumu yao.

Naye Naibu Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Mcha Hassan Mcha, amewataka watumishi wa TRA kuendelea kuboresha huduma kwa walipakodi, kutanua wigo wa walipakodi na kupambana na njia mbalimbali za ukwepaji wa kodi.

Amewapongeza watumishi wa TRA kwa kuendelea kufanya kazi na bidi hali iliyowawezesha kuvuka malengo kwa miezi 18 mfululizo huku ikiweka rekodi ya juu kabisa ya makusanyo kwa kukusanya kiasi cha Sh. Trilioni 4.13 kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Raslimali Watu na utawala wa TRA Bw. Moshi Jonathan Kabengwe amewapongeza wajumbe walioshiriki mkutano huo huku akiwataka kuzingatia yale yote waliyokubaliana katika mkutano huo ili TRA iendelee kuvuka malengo ya Makusanyo.

Aidha, amewapongeza watumishi wa TRA wanaotarajiwa kustaafu ndani ya mwaka huu wa 2026 huku akisema kuwa watumishi hao wameacha alama katika utendaji wao wa kazi.

Mkutano huo wa Siku 5 wa kutathmini utendaji kazi wa TRA kwa Nusu ya Kwanza ya Mwaka wa fedha 2025/26 umeshirikisha jumla ya washiriki 477 kutoka katika ofisi za TRA nchi nzima.



No comments