FCC YAPONGEZWA KWA KUDHIBITI BIDHAA BANDIA, YATAKIWA KUONGEZA NGUVU



Uwepo wa Tume ya Ushindani Tanzania-FCC, umetajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa uingizaji na usambazaji wa bidhaa bandia katika maeneo mbalimbali ya nchi, hususan bandarini na mipakani.

Serikali imeipongeza FCC kwa juhudi zake za kuimarisha usimamizi na ukaguzi wa bidhaa hizo, hatua inayolenga kulinda afya za watumiaji na kukuza ushindani wa haki katika soko.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, alipokuwa akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, katika ufunguzi wa kikao kazi kati ya FCC na Jukwaa la Wahariri Tanzania-TEF kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Mpogolo, amesema mafanikio yaliyopatikana yanaonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za serikali na wadau wengine, wakiwemo wanahabari, katika vita dhidi ya bidhaa bandia.

Hata hivyo, ameitaka FCC kuongeza juhudi zaidi, hasa katika maeneo yenye shughuli kubwa za kibiashara kama Soko Kuu la Kimataifa Kariakoo na maeneo mengine ya Jiji la Dar es Salaam, ambako bado kuna changamoto ya uwepo wa bidhaa zisizo halali sokoni.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa FCC, Amina Ngasongwa, amepongeza mchango wa vyombo vya habari katika kuelimisha umma kuhusu madhara ya bidhaa bandia na umuhimu wa kuzitambua kabla ya kununua.

Kikao kazi hicho kililenga kuimarisha ushirikiano kati ya FCC na wahariri wa vyombo vya habari ili kuongeza uelewa wa umma na kuendeleza mapambano dhidi ya bidhaa bandia.






No comments