FOUNTAIN GATE YAHAMIA RASMI JIJINI ARUSHA
Mkuu wa Mkoa wa Arusha CPA Amos Gabriel Makalla amewaomba wananchi wa Mkoa wa Arusha kuipokea na kuipa ushirikiano Timu ya mpira wa miguu ya Fountain Gate inayoshiriki Ligi kuu Tanzania bara na iliyohamia Mkoani Arusha kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid kama uwanja wake wa nyumbani kwenye ligi kuu.
Makalla ametoa wito huo leo Ijumaa Februari 06, 2026 alipoongoza mapokezi ya Timu hiyo ikitokea Mkoani Manyara, akisema ujio wa Timu hiyo Mkoani hapa kutasisimua uchumi wa wananchi na kuongeza mnyororo wa thamani utakaowagusa wajasiriamali na wafanyabiashara wa Mkoa wa Arusha.
"Niwaombe wananchi wa Mkoa wa Arusha muipokee timu hii na katika utalii wa michezo, Fountain Gate ikiwa hapa, timu zote za ligi kuu zitakuja hapa maana yake bodaboda atafaidika, Mama ntilie atafaidika, kwenye masoko watafaidika na Mahoteli yetu yatajaa na hivyo sote tutanufaika na mpango wangu ni kuwa na Timu mbili hapa za Ligi kuu Tanzania bara." Amesema Makalla.
Makalla ameahidi pia kutoa Milioni 20 kwa timu hiyo kusaidia uendeshaji na kutoa motisha kwa wachezaji, akiwaomba wadau na Makampuni kuweza kufanya kazi na kuwekeza kwenye timu hiyo, akiahidi pia kushirikiana na Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha ili kuuboresha uwanja wa Sheikh Amri Abeid uweze kufungwa taa ili uweze kutumika kwa michezo ya usiku.
Kwa upande wake Rais wa Klabu hiyo ya Fountain Gate Japhet Mboto Makau, amemshukuru Mhe. Makalla kwa mapokezi yake na kukubali kwake kuwa mlezi wa timu hiyo, akisema wamekuja Arusha kuiheshimisha na kuendeleza heshima ya mpira wa miguu Mkoani Arusha iliyowekwa miaka ya nyuma.
Post a Comment