MAFUNZO YA SIKU TANO KWA WATAALAM WA MAABARA NCHINI YAKAMILIKA KWA MAFANIKIO


Wizara ya Afya kupitia Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii (NPHL) imetoa mafunzo ya vitendo kwa wataalam wa maabara 40 kutoka hospitali mbalimbali za ngazi ya Mkoa na Kanda nchini, kwa lengo la kuimarisha uwezo wao wa kutambua na kuthibitisha vimelea vinavyosababisha ugonjwa wa kipindupindu kwa usahihi na kwa wakati.


Akizungumza leo Machi 13, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, Bw. Ambele Mwafulango amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuimarisha mifumo ya uchunguzi wa maabara ili kuhakikisha majibu ya vipimo yanapatikana kwa haraka na kwa usahihi.


Bw. Mwafulango amesema wataalam hao wamefundishwa mbinu za kisayansi za kuchukua sampuli, kufanya uchunguzi wa maabara pamoja na kuthibitisha uwepo wa vimelea vinavyosababisha kipindupindu, hatua itakayosaidia kutoa taarifa sahihi kwa mamlaka za afya na kuwezesha hatua za haraka za kudhibiti ugonjwa huo.


Kwa mujibu wa waandaaji wa mafunzo hayo, uboreshaji wa uwezo wa wataalam wa maabara ni muhimu ili kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa na kusaidia mamlaka za afya kuchukua hatua stahiki mapema pindi milipuko ya magonjwa inapojitokeza katika jamii.


Aidha, Bw. Mwafulango amesisitiza kuwa wataalam hao wanatarajiwa kutumia maarifa waliyoyapata ndani ya vituo vyao vya kazi ili kuboresha ubora wa huduma za uchunguzi wa maabara na kuchangia utoaji wa taarifa sahihi za kiafya kwa ajili ya kulinda afya ya wananchi.


Ameongeza kuwa mafunzo hayo pia yanalenga kuongeza utayari wa nchi katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, hususan kipindupindu, kwa kuhakikisha huduma za uchunguzi wa maabara zinakuwa sahihi, za haraka na zenye kuaminika.


Mafunzo hayo ya siku tano yalianza Machi 9 na kuhitimishwa Machi 13, 2026, yakihusisha wataalam wa maabara kutoka maeneo mbalimbali nchini waliopatiwa mbinu za kisasa za uchunguzi wa vimelea vinavyosababisha magonjwa ya mlipuko.

No comments