WAZABUNI RUVUMA, IRINGA NA NJOMBE WAJENGEWA UWEZO MATUMIZI YA MODULI YA RUFAA


Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), imewakutanisha wazabuni na Taasisi Nunuzi wa mikoa ya Ruvuma, Iringa na Njombe na kuwajengea uwezo kuhusu Moduli ya kupokea na kushughulikia Malalamiko na rufaa kwenye mfumo wa NeST kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi. 


Mafunzo hayo yamefanyika kwa nyakati tofauti katika miji ya Songea na Iringa yamewahusisha washiriki 380 ambao ni wazabuni, wataalamu wa ununuzi, sheria, Tehama pamoja na makundi maalum yakiwemo wanawake, vijana, wazee na watu wenye mahitaji maalum pamoja na mafundi wa ndani.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Katibu Mtendaji wa PPAA,James Sando amesema mafunzo hayo yamekuwa yakitolewa na PPAA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa lengo la kuwajengea uwezo wazabuni na Taasisi Nunuzi ili kuwapa ufanisi zaidi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, hususan katika kushughulikia malalamiko na migogoro itokanayo katika michakato ya ununuzi wa Umma. 


Sando ameongeza kuwa, katika kutimiza azma ya Serikali mafunzo yamewashirikisha vijana, wanawake na makundi maalum katika ununuzi wa umma ili kuwawezesha kupata elimu kuhusu ununuzi wa Umma hususan katika michakato ya ununuzi na kuhakikisha kuwa wanaisaidia Serikali kupata thamani halisi ya fedha katika miradi ya kimkakati yenye tija kwa Taifa.  


Pamoja na mambo mengine, amewasihi washiriki kutumia mafunzo hayo kujifunza namna moduli ya kuwasilisha malalamiko na rufaa inavyofanya kazi katika Mfumo wa NeST kwani inatoa njia rahisi, ya haraka na yenye uwazi kwa wadau wote kushiriki katika mchakato wa ushughulikiaji wa malalamiko yanayotokana na michakato ya zabuni za umma. 


Kwa upande wake Meneja wa Usimamizi wa Rufaa na Sheria (PPAA), Florida Mapunda amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kutoa elimu kwa wadau wa ununuzi wa Umma kuhusu taratibu za uwasilishaji na ushughulikiaji wa malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST. 


Mapunda ameongeza kuwa tangu kuanza kwa matumizi ya Moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST, takribani mashauri 596 yamewasilisha kupitia mfumo huo, jambo linaloifanya Mamlaka ya Rufani kuendelea kutoa elimu kwa wadau wa ununuzi wa umma ili waweze kufahamu namna sahihi ya matumizi ya moduli hiyo.


Kupitia mafunzo hayo, mada mbalimbali zimewasilishwa ikiwemo  uwasilishaji na ushughulikiaji wa malalamiko na rufaa katika ununuzi wa umma, uwasilishaji na ushughulikiaji wa malalamiko katika mfumo wa NeST, utoaji wa tuzo, uandaaji, upekuzi, na utiaji saini wa mkataba. 


Mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo ya awali yaliyofanyika katika Kanda ya Pwani, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na Kanda ya Kati, mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Mwanza, Kilwa, Lindi na Mtwara









No comments