JKCI KUFUNGUA TAWI DRC CONGO
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete-JKCI, imepanga kuvuka mipaka ya nchi na kufungua tawi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo katika kutoa huduma bingwa bobezi za matibabu ya moyo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi mtendaji wa JKCI, Dokta Peter Kisenge wakati wa ziara ya Gavana wa jimbo la Maniema la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC, Mussa Kabwankubi Moise alipotembelea JKCI, jijini Dar es Salaam.
Dokta Kisenge, amesema JKCI inataka kusogeza huduma za matibabu ya moyo kwa wananchi wa Congo kuwapunguzia adha ya kusafiri umbali mrefu kwenda katika mataifa ya mbali kupata huduma hizo.
Kwa upande wake, Gavana wa jimbo la Maniema la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mussa Kabwankubi Moise, amesema baada ya kutembelea Taasisi hiyo ameridhishwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Tanzania na kuifanya JKCI kuwa kinara katika utoaji wa huduma bingwa bobezi za upasuaji wa moyo Afrika Mashariki na kati.
Naye, Balozi wa Tanzania katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC, Juma Mshana, ameipongeza menejimenti ya Taasisi hiyo kwa kushirikiana vema na nchi ya Congo katika kuimarisha uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi hizo mbili.


Post a Comment