MPAKA WA TUNDUMA NI LANGO MUHIMU LA KIUCHUMI TANZANIA - WAZIRI KOMBO



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amefanya ziara katika Kituo cha Pamoja cha Mpaka wa Tunduma (OSBP) mkoani Songwe tarehe 23 Februari 2026. Ziara hiyo imelenga kukagua maendeleo ya miundombinu na utekelezaji wa huduma za pamoja kati ya Tanzania na Zambia ili kurahisisha biashara na usafirishaji wa mizigo na abiria.


Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameeleza kuwa Mpaka wa Tunduma ni lango muhimu la kiuchumi kati ya Tanzania na Zambia, lenye mchango mkubwa katika kukuza biashara ya kikanda na pato la Taifa. Alibainisha kuwa maboresho ya miundombinu yanayoendelea yataongeza kasi ya biashara na kupunguza gharama za usafirishaji mpakani hapo.


Kwa upande wa TRA kama taasisi mama inayosimamia mpaka huo imewakilishwa na Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Songwe, CPA Saidi Mwamloso, pamoja na Meneja wa Forodha Tunduma, Bw. Nsajigwa Mwambegele, ambao wameshiriki kikamilifu katika mapokezi na kutoa maelezo kuhusu maboresho ya huduma za forodha na maendeleo yanayoendelea katika kituo hicho cha mpakani.


Bw. Mwambegele ameeleza kuwa maboresho ya huduma na miundombinu yanayoendelea kituoni hapo, yanalenga kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za forodha kwa kuimarisha matumizi ya mifumo ya kisasa na uratibu wa pamoja kwa taasisi zinazohudumu mpakani 

No comments