SERIKALI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA WADAU KUKUZA HUDUMA ZA KITALII NCHINI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb.) amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi, taasisi za kifedha pamoja na wadau wengine kuhakikisha mifumo ya malipo ya kidigitali inaendelea kuimarika na kuwa na manufaa kwa wananchi na wageni wanaotembelea hapa nchini

Mhe. Chande amebainisha hayo Jijini Arusha wakati wa hafla ya kuzindua huduma ya Azampesa kwa kushirikiana na Visa kwa malipo ya kidijitali kwa watalii wa kimataifa na kutoa wito kwa mashirika mengine kuwa wabunifu kubuni njia bora na za kisasa katika utoaji wa huduma kwa watalii wanaotembelea hapa nchini ili kutoa fursa za ajira kwa vijara na ukuaji wa uchumi wa taifa

“Huduma hii italeta manufaa makubwa, ikiwa ni pamoja na kuimarisha uzoefu wa watalii wanaotembelea Tanzania kwa kuwapatia huduma za malipo zilizo rahisi, salama na za kisasa, kuwawezesha wafanyabiashara wa ndani, kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidigitali, kuongeza uwazi na ufanisi katika miamala ya kifedha, sambamba na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya taifa” Alifafanua Mhe. Chande
Mhe. Chande ameongezea kuwa huduma ya Azampesa imekuja wakati mwafaka hususan katika kipindi hiki cha uongozi thabiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo sekta ya utalii imezidi kuimarika kwa kasi. Kati ya mwaka 2021 na 2025 idadi ya watalii wa ndani imeongezeka kutoka 788,933 mwaka 2021 hadi million 3.6 mwaka 2025, huku watalii wa kimataifa wakiongezeka kutoka 922,692 hadi million 2.2 katika kipindi kama hicho ikiwa ni matokeo ya filamu za Royal Tour na Amizing Tanzania.

Katika hatua nyingine Mhe. Chande ameelekeza watoaji wa huduma hiyo licha ya kutumia lugha ya kigeni katika mfumo wa kujisajili pia watumie lugha ya Kiswahili ili kuenzi na kuthamini utaifa wetu. Aidha, amewaasa kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa huduma hiyo na kuimarisha ulinzi na usalama wa mifumo sambamba na kujipanga vema kuhudumia wageni wakati wa Michuano ya AFCON 2027, kipindi ambacho tunategemea kuwa na wageni wengi nchini.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu AzamPesa, Bw. Firas Ahmad mesema malipo digitali yanalenga kuwawezesha watalii kufanya miamala kwa urahisi kote Tanzania bila hitaji la fedha taslimu, ATM au matumizi ya kadi halisi ambapo huduma hiyo ni suluhisho la malipo kwa watalii Tanzania.

Naye Makamu wa Rais na Meneja Mkuu wa Visa Afrika Mashariki Bw. Chad Pollock amefafanua kuwa kupitia ushirikiano na AzamPesa, Visa itawezesha wamiliki wa kadi za Visa kufanya malipo kama wenyeji kupitia simu zao za mkononi. 

Ushirikiano kati ya AzamPesa na Visa umekuja na kaulimbiu isemayo “Pay Like Local” ili kuwarahisishia watalii kupata huduma mbalimbali lakini pia kuwawezesha wafanyabiashara kuuza bidhaa zao kwa urahisi.

No comments