CG MWENDA AKUTANA NA UONGOZI WA HOSPITALI YA BENJAMINI MKAPA



Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda leo tarehe 01.03.2026, amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Hospitali ya Benjamini Mkapa wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo Prof. Abel Makubi katika ofisi za TRA jijini Dar es Salaam.


Katika mazungumzo hayo Kamishna Mkuu Mwenda ameipongeza Hospitali ya Benjamini Mkapa kwa kulipa kodi kwa hiari na kuendelea kutoa huduma bora za afya kwa watanzania zinazoonyesha thamani ya serikali kuwekeza katika sekta ya afya.


Amesema miongoni mwa huduma zinazowekezwa na Serikali kupitia kodi na kugusa wananchi wengi ni huduma za afya ikiwemo Hospitali ya Benjamini Mkapa huku akiweka wazi kuwa TRA ipo tayari kuisaidia hospitali hiyo katika mfuko wa matibabu ya wagonjwa 100 wanaotarajiwa kupandikizwa Figo na Uloto kwa watoto wenye Seli Mundu kwa kuchangia kiasi cha kufanikisha matibabu hayo.


Aidha Kamishna Mkuu Mwenda amesema Hospitali ya Benjamini Mkapa ni miongoni mwa walipakodi wazuri ambao wamekuwa wakilipa kodi kwa uaminifu na kuwa TRA ipo kuwezesha walipakodi wote kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kuwafanya wale wasiolipa kodi waanze kulipa ili kuchangia maendeleo ya Taifa na kuiwezesha Tanzania kujitegemea kiuchumi kwa kiasi kikubwa.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamini Mkapa Prof. Abel Makubi ameipongeza TRA kwa kuwa karibu na wananchi na kuwafanya waone kulipa kodi ni wajibu wao hali ambayo imeongeza makusanyo ya kodi ambazo zinakwenda kuisaidia nchi.


Amesema Hospitali ya Benjamini Mkapa ni miongoni mwa wanufaika wa kodi huku akieleza huduma za kibingwa wanazotoa ikiwemo kupandikiza uloto kwa wagonjwa Seli Mundu na kupandikiza Figo hali ambayo imefanya wahitaji wa huduma hizo kutibiwa nchini huku mataifa mengine wakija nchini kufuata huduma hizo za kibingwa.

No comments