HEDHI SALAMA INAHITAJI UWAZI, ELIMU, USHIRIKIANO WA JAMII


Hedhi ni miongoni mwa mambo yanayohitaji uelewa sahihi, mazungumzo ya wazi na ushirikiano wa jamii ili kuhakikisha wasichana na wanawake wanapata huduma na mazingira salama wakati wote wa hedhi.


Hayo yameelezwa  leo Machi 02, 2026  mkoani Morogoro  na Mkuu wa Sehemu Ndogo ya Afya Mazingira kutoka Wizara ya Afya, Bw. Anyitike Mwakitalima wakati wa Mafunzo kwa Wawezeshaji ngazi ya Taifa (NToTs) kuhusu Mwongozo wa Hedhi Salama na Zana zake yaliyoandaliwa na Idara ya Kinga.


Bw. Mwakitalima, amesema ni muhimu jamii kuondoa unyanyapaa na dhana potofu kuhusu suala la hedhi ili kulinda afya na heshima ya wasichana na wanawake.


“Masuala ya hedhi ni nyeti hivyo lazima yazungumzwe ili jamii ipate uelewa sahihi kuhusu hedhi salama kwani Bila Hedhi Salama Hakuna Maisha, jamii kwa ujumla wake ishiriki kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata huduma bora na endelevu za Hedhi Salama", amesisitiza Bw. Mwakitalima.


Mwakitalima amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo Wawezeshaji wa Kitaifa (NToTs) ili waweze kusambaza mwongozo huo kwenye mikoa na Halmashauri zote nchini na kuhakikisha utekelezaji wake unaleta matokeo chanya kwa ustawi wa jamii yenye afya bora. 


Kwa upande wake, mwakilishi kutoka UNICEF Bi. Regnihaldah Mpete akizungumza kwa niaba ya wadau wa maendeleo,  ameipongeza Wizara ya Afya kwa kuandaa mwongozo huo na kuukamilisha, akisema ni hatua muhimu katika kuimarisha usimamizi wa hedhi salama, kuboresha afya ya mazingira na kulinda ustawi wa jamii kwa ujumla.


"Ninaamini mafunzo haya yanatarajiwa kuongeza uelewa, kuimarisha ushirikiano wa sekta mtambuka na kuhakikisha mwongozo wa hedhi salama unatekelezwa kwa ufanisi nchini nzima," amesema Bi. Mpete.









No comments