HONGERA TANESCO KUWAFIKIA WANAWAKE KWA NISHATI SAFI YA UMEME – WAZIRI DKT. GWAJIMA

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme inayolenga kubadili mtazamo wa jamii na kuongeza matumizi ya umeme katika shughuli za kila siku, hususan kupikia.

Amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni nyenzo muhimu ya kumkomboa mwanamke, kuboresha afya za familia na kuchochea maendeleo ya uchumi wa kaya.

Dkt. Gwajima ametoa kauli hiyo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Pili la Wanawake wa TANESCO linalolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambalo, limewakutanisha wanawake wa TANESCO kutoka mikoa yote nchini tarehe 4 Machi 2026 jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Diamond Jubilee

Akizungumza katika kongamano hilo, Waziri Gwajima amesema, takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 zinaonesha kuwa, zaidi ya 81% ya kaya nchini bado zinatumia kuni na mkaa, hali inayowaweka wanawake katika hatari kubwa ya magonjwa ya mfumo wa hewa na kuchangia uharibifu wa mazingira. 
Alibainisha kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kinara wa ajenda ya nishati safi Afrika, imeweka ajenda ya nishati safi ya kupikia kuwa kipaumbele cha kitaifa, ikilenga kuhakikisha 80% ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.

Dkt. Gwajima ameeleza kuwa, maendeleo ya teknolojia yameleta majiko yanayotumia umeme kidogo kwa gharama nafuu, ambapo, mlo mmoja unaweza kupikwa kwa chini ya uniti moja ya umeme. 

Aidha, ameipongeza TANESCO kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya umeme na kubuni programu bunifu za kuongeza matumizi ya umeme kwa kupikia, huku akitoa wito kwa wanawake wa TANESCO kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii. Katika hatua nyingine, ameahidi kuwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa TANESCO kupitia kampeni za uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, akisisitiza kuwa ajenda hiyo inagusa moja kwa moja maendeleo ya jamii, hususan wanawake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema, lengo la kampeni hiyo ni kubadili mtazamo wa jamii na kuongeza matumizi ya umeme katika shughuli za kila siku, hususan kupikia. 

Amesisitiza kuwa, TANESCO itaendelea kuzingatia usawa wa kijinsia katika utekelezaji wa mipango na miradi yake ili kuendana na malengo ya Dira ya Taifa ya 2050, pamoja na kukuza ushiriki wa wanawake katika sekta ya nishati.

Naye Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa TANESCO, Margareth Mwandu, ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira wezeshi na kumpongeza Waziri Gwajima kwa kuwa kinara wa ajenda za uwezeshaji wa wanawake na usawa wa kijinsia. 

Amesema msukumo huo umeongeza ari na kutoa fursa zaidi kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taasisi na taifa kwa ujumla.

No comments