KAMATI YA BUNGE NISHATI NA MADINI YARIDHISHWA MAENDELEO YA KIWANDA CHA NGUZO ZA ZEGE
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeridhishwa na Ujenzi wa Kiwanda cha Zege kinachomilikiwa na kampuni tanzu ya TANESCO ya kuzalisha nguzo za zege kilichopo katika Mkoa wa Tabora wakati wa ziara yao ya kikazi Mkoani humo tarehe 12 Machi, 2026.
Akizungumza baada ya ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Subira Mgallu ameeleza kuridhishwa na hatua ya kukamilika kwa Kiwanda hicho kilichoanza uzalishaji na kuwaelekeza Wizara ya Nishati na TANESCO kukisimamia kiwanda hiko kiendelee kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kuzalisha faida.
Alieleza kuwa uelekeo wa sasa ni kusambaza nguzo za zege hasa kwa maeneo yenye unyevu sambamba na maeneo yaliyo karibu na misitu pamoja na mikondo ya mito ya maji ambayo nguzo za miti huathirika kwa kiasi kikubwa haswa kwenye msimu wa mvua hivyo nguzo za zege zitakuwa msaada mkubwa katika mazingira kama hayo na kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme.
Naye, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema ujenzi wa kiwanda hiko umekamilika mwaka huu na kuanza uzalishaji wake rasmi Februari, 2026 ambapo mpaka sasa wastani wa nguzo zinazozalishwa ni 80 hadi 120 kwa siku ambapo mpaka sasa gharama ya shilingi bilioni 6.4 imeshatumika katika hatua zote hadi uzalishaji ulipoanza ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1.4 bado hazijalipwa kwa mkandarasi ambaye bado yupo kwenye kipindi cha uangalizi.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, ameeleza kuwa kukamilika kwa kiwanda hiko kunaenda kuleta mageuzi makubwa kwani nguzo za zege ni teknolojia ambayo bado inakuwa hivyo Shirika bado linaendelea kuikuza sekta na kuwa na utoshelevu wa nguzo zenyewe kwa matumizi ya wananchi.
Post a Comment