KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA UWANJA WA ARUSHA

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo wakiongozwa na Mwenyekiti Husna Juma Sekiboko (Mb), leo tarehe 12 Machi 2026 wametembelea mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Kimataifa unaoendelea kujengwa jijini Arusha.

Katika ziara hiyo, wajumbe hao wamepokelewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Paul Christian Makonda ambapo walipata fursa ya kukagua hatua za utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kimichezo ulioanza mwaka 2024.

Baada ya ukaguzi huo, Kamati imeeleza kuridhishwa na kasi ya maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo na kupongeza jitihada zinazofanywa na Serikali kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa, ambao ni mwezi Julai 2026.

Aidha, wajumbe wa Kamati hiyo wamempongeza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa sekta ya michezo kwa kutenga fedha za kutosha ili kuhakikisha mradi huo muhimu unakamilika na kuleta tija kwa maendeleo ya michezo nchini.

Mradi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Kimataifa wa Arusha unatekelezwa na kampuni ya China Railway Construction Engineering Group Limited kwa gharama ya Shilingi bilioni 286 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania. Uwanja huo unatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya miundombinu itayotumika katika mashindano ya Africa Cup of Nations (AFCON) ambayo yatafanyika mwaka 2027.

No comments