SERIKALI, WADAU WAENDELEA KUIMARISHA AFYA YA UZAZI NA AFYA YA VIJANA SHULENI

 


Serikali kupitia Wizara ya Afya pamoja na wadau imeendelea kusisitiza dhamira ya kuimarisha huduma za afya ya uzazi, afya ya mama na mtoto pamoja na afya ya vijana balehe nchini.


Hayo yameelezwa leo Machi 13, 2026 na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dkt. Ahmed Makuwani, wakati wa kikao cha mapitio ya mwaka cha programu ya kuongeza huduma za uzazi wa mpango kinachotekelezwa kwa ushirikiano na EngenderHealth Tanzania, kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Afya jijini Dodoma.


Dkt. Makuwani amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa EngenderHealth Tanzania katika kusaidia utekelezaji wa afua mbalimbali za afya, ikiwemo kuboresha huduma za afya ya uzazi, kuimarisha programu ya afya shuleni pamoja na kuongeza upatikanaji wa bidhaa za uzazi wa mpango katika vituo vya kutolea huduma za afya.


Ameongeza kuwa Serikali pia inawashukuru washirika wa maendeleo, wakiwemo Foreign, Commonwealth & Development Office (FCDO) pamoja na British High Commission, kwa msaada wao wa kifedha na kiufundi unaochangia kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini.


Kwa upande wake, Mratibu wa Afya Shuleni kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Joyce Sigalla, ameishukuru Wizara ya Afya kwa ushirikiano wake kupitia ufadhili wa EngenderHealth Tanzania katika kuandaa Mwongozo wa Vilabu vya Afya na Lishe Shuleni.


Dkt. Sigalla amesema mwongozo huo utasaidia kuongeza uelewa kwa wanafunzi kuhusu masuala ya afya na lishe, kuzuia mimba za utotoni, pamoja na kuhakikisha kila mwanafunzi anapata fursa sawa ya kushiriki katika vilabu vya afya shuleni












No comments