WIZARA YA AFYA YAWANOA WATAALAMU WA MAABARA 45 KUIMARISHA UFUATILIAJI WA VIMELEA
Wizara ya Afya kupitia Mradi wa Usalama wa Afya Duniani imeendesha mafunzo ya ufuatiliaji wa vimelea katika mazingira ya kutolea huduma za afya kwa wataalamu wa maabara 45 kutoka hospitali za rufaa za mikoa yote nchini.
Akielezea kuhusu mafunzo hayo yaliyofanyika mkoani Morogoro Machi 11, 2026 Afisa kutoka Kitengo cha Uhakiki wa Ubora wa Huduma za Afya Wizara ya Afya, Bi. Ruth Raymond amesema mafunzo hayo yanaimarisha afua za kinga na udhibiti wa maambukizi.
Bi. Ruth amesema mafunzo hayo yamelenga kuwaongezea uwezo wataalamu hao kwa kukusanya, kuhifadhi na kuchambua sampuli kutoka kwenye mazingira mbalimbali kwa usahihi ili kutambua mapema uwepo wa vimelea hatarishi.
Amefafanua kuwa, hatua hiyo itasaidia kupunguza maambukizi yatokanayo na huduma za afya na kuwawezesha wataalam kufanya maamuzi ya kitaalamu yanayolinda usalama wa wagonjwa.
Kwa upande wake, Profesa Mtebe Majigo kutoka Muhimbili University of Health and Allied Sciences (MUHAS) amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo wafanyakazi wa maabara kushughulikia changamoto ya usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa za antibayotiki (UVIDA).
Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa Mradi wa Usalama wa Afya Duniani, Dkt. Sirio Kulaya, amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya wameendelea kuboresha miundombinu ya afya ili kuzuia na kudhibiti usambaaji wa vimelea vinavyoweza kusababisha magonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Kwa upande wa washiriki wa mafunzo hayo, Doreen Philip, mtaalamu wa maabara kutoka National Health Laboratory, amepongeza mafunzo hayo akisema yamekuwa na matokeo chanya katika kuwajengea wataalamu wa maabara ujuzi na uwezo wa kufanya kazi kwa weledi na ufanisi.

Post a Comment